WADAU WA PROGRAMU YA MMMAM WAKUTANA MOROGORO KUANDAA MPANGO KAZI
Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
WADAU wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT–MMMAM) wamekutana mkoani Morogoro kuandaa mpango kazi wa programu hiyo utakaotumika katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.
Akizungumza katika kikao hicho, Mratibu wa Huduma za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Afya ya Uzazi wa Mama na Mtoto, Ephrahim Kafilimbi, alisema mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha elimu ya malezi katika ngazi zote za msingi.
Kafilimbi alibainisha hayo wakati akifungua kikao kazi cha siku nne cha wadau wa MMMAM kinachoendelea mkoani Morogoro.
Aidha, alisema mpango huo umelenga pia kuanzisha huduma za kona za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika vituo vya afya na maeneo yote ya kutolea huduma za afya.


