HOFU YA MAJI MINDU YATOWEKA BAADA YA AJALI YA KEMIKALI
Matukio Daima, Morogoro
Hofu iliyokuwa imetanda kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro kuhusu usalama wa maji ya Bwawa la Mindu baada ya kutokea kwa ajali ya gari iliyokuwa ikisafirisha Kemikali aina ya Sulphur imeanza kutoweka, baada ya mamlaka husika kuthibitisha kuwa maji hayo ni salama kwa matumizi.
Ajali ya lori lililokuwa linasafirisha kemikali ya sulphur iliyomwagika karibu na bwawa hilo, eneo la Mtaa wa Mikoroshini, Kata ya Mindu Manispaa ya Morogoro, katika barabara kuu ya Morogoro-Iringa ilizua wasiwasi mkubwa, hasa ikizingatiwa kuwa zaidi ya asilimia 75 ya wakazi hutegemea chanzo hicho kupata Maji safi na salama.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Moruwasa, CPA Sais Kyejo, amesema hakuna madhara yoyote yaliyobainika katika ubora wa maji yanayosambazwa na Wala Kemikali hiyo haikufikia kabisa Maji yanayozalishwa kutoka Bwawa Hilo.
Akawasihi wananchi waendelee kutumia maji bila hofu kwani tathmini ya awali imebainisha hakuna athari yoyote iliyojitokeza.
Mkurugenzi wa Maji Bonde la Wami Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmasi, amesema Mindu ni salama baada ya juhudi za haraka zilizofanywa na wataalamu kutoka mamlaka mbalimbali kusaidia kuzuia kemikali hiyo isisambae eneo lolote ikiwemo kwenye chanzo hicho maji.
Mhandisi Mmasi akatumia nafasi hiyo kuwasihi madereva kuwa makini barabarani na wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona ajali, hasa zinazohusisha vitu hatarishi.
Kwa upande wake, Bi Magdalena Mtenga, Meneja wa Kanda ya Kati,Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali amesema kemikali hiyo inaweza kuwa hatari endapo itashughulikiwa bila tahadhari, lakini hadi sasa hakuna madhara yaliyoripotiwa kwa wananchi.
Akasema Kemikali hiyo inatabia ya kushika moto na kulipuka, mambo ambayo hayakutokea wakati wa kuiondoa eneo hilo usiku na mchana, na tabia nyingine ni kuwasha kwenye mwili au kukereketa kooni.
Hata hivyo akasema kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali ikiwemo Bonde la Wami Ruvu, Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Morogoro MORUWASA, Baraza la Usimamizi wa Mazingira NEMC na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na wameondoa Kemikali hiyo katika eneo la Ajali.
Naye Meneja wa NEMC Kanda ya Morogoro na Rufiji, Arnold Mapinduzi, amesema kemikali hiyo inaondolewa kwa usalama na itateketezwa kwa mujibu wa sheria ili kulinda mazingira.
Ajali hiyo ni ya tatu ndani ya mwezi mmoja ikuhusisha usafirishaji wa kemikali aina ya sulphur mkoani Morogoro jambo lililousukuma ofisi ya maabara ya mkemia mkuu wa Serikali Kanda ya Kati kufikiri mapendekezo ya kusafirisha aina hiyo ya Kemikali kwa kusindikizwa (escorts) kama ilivyo kwa Kemikali nyingine hatarishi.




