TASAC YATOA ONYO KALI DHIDI YA USAFIRISHAJI WA WAHAMIAJI HARAMU
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa onyo kali kwa taasisi na mawakala wa meli nchini kujiepusha na vitendo vya kusafirisha wahamiaji haramu, likisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayehusika.
Onyo hilo limetolewa na Ofisa Mfawidhi wa TASAC kwa mikoa ya Mtwara na Lindi, Mhandisi Joseph Myaka, kufuatia tukio la hivi karibuni la kukamatwa kwa wahamiaji haramu katika ukanda wa Kusini. Amesema TASAC haitavumilia ukiukwaji wa sheria za usafirishaji wa baharini na imejipanga kuhakikisha nidhamu na usalama vinaimarishwa katika sekta hiyo.
Katika tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, limefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 70 waliokuwa wakisafirishwa kwa njia ya bahari.
Wahamiaji hao walikutwa ndani ya chombo kilichotambulika kwa jina la FS Sae Mfalme, kinachodaiwa kumilikiwa na mtu anayejulikana kwa jina la Bw. Njomo. Taarifa za awali zinaeleza kuwa walikuwa wakitokea Mombasa, Kenya wakielekea nchini Comoro kinyume cha taratibu za uhamiaji.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, ACP John Imori, alisema tukio hilo lilitokea Machi 31 majira ya saa 10 usiku katika Bandari ya Kilwa Masoko, wilayani Kilwa. Alibainisha kuwa kati ya wahamiaji hao, 10 ni wanawake na 60 ni wanaume.
Mamlaka husika zimeendelea na uchunguzi wa tukio hilo huku hatua za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa dhidi ya wahusika wote. TASAC imesisitiza kuwa ushirikiano kati ya taasisi za serikali na wadau wa sekta ya usafirishaji ni muhimu katika kukomesha vitendo hivyo vinavyohatarisha usalama wa mipaka na maisha ya binadamu.

