Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
SERIKALI YAHIMIZA WASICHANA KUSOMA TEHAMA ILI KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIDIGITALI

SERIKALI YAHIMIZA WASICHANA KUSOMA TEHAMA ILI KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIDIGITALI

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma


NAIBU Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Mkama, amesisitiza umuhimu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kurahisisha utendaji wa kazi na kufungua fursa mbalimbali za maendeleo, hasa kwa vijana wa kike.


Akizungumza katika Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wasichana katika  TEHAMA, Dkt Mkama amesema kuwa nchi nyingi duniani zimeendelea kuhamasisha wasichana kusoma masomo ya TEHAMA ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidigitali. 


Ameeleza kuwa TEHAMA inamwezesha kijana kufanikiwa katika masomo, ajira pamoja na ubunifu wa fursa mpya.


Aidha, ametoa wito kwa wakuu wa shule na vyuo nchini Tanzania Bara na Zanzibar kuanzisha klabu za kidigitali zitakazosaidia kuwaandaa wanafunzi, hususan wasichana, kukabiliana na ushindani wa kimataifa katika sekta ya teknolojia.

Hata hivyo, Dkt. Mkama amesisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo endelevu wa kuwafuatilia na kuwaendeleza washindi wa mashindano ya TEHAMA, badala ya kuwaacha baada ya kupokea zawadi, ili kuhakikisha vipaji vyao vinaendelea kukuzwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Jabiri Bakari, amesema kuwa matumizi ya Akili Bandia (AI) yameongezeka kwa kasi duniani kutokana na maendeleo ya teknolojia, ikiwemo uwezo mkubwa wa kukusanya na kuchakata taarifa.

Amebainisha kuwa AI si teknolojia mpya, bali ilianza tangu miaka ya 1950, lakini kwa sasa imepata nguvu zaidi na imekuwa sehemu ya mifumo mingi ya kidigitali, ikiwemo huduma za simu tunazotumia kila siku.

Mhandisi Bakari amesema wasichana wana nafasi kubwa katika sekta ya TEHAMA, hasa katika kubuni suluhisho na ubunifu wa kiteknolojia, na hivyo wanapaswa kuchangamkia fursa za kujifunza ili kuwa sehemu ya kizazi cha kidigitali.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Ulanga, amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya miradi ya UCSAF inayotekelezwa tangu mwaka 2016 kwa lengo la kuongeza uelewa wa TEHAMA nchini.

Amesema kwa mwaka huu, jumla ya wanafunzi 281 wamepatiwa mafunzo hayo, huku wanafunzi 31 wakifanikiwa kufika ngazi ya kitaifa kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

Naye mnufaika wa mafunzo hayo, Beatrice Chrispine, amewahimiza wasichana kuondoa hofu ya kusoma masomo ya TEHAMA na badala yake kujitokeza kwa wingi kuyasoma, 

Ameeleza kuwa kupitia TEHAMA, mtu anaweza kupata fursa nyingi za ajira na hata kazi kumfuata yeye mwenyewe.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3