Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
POLISI MOROGORO, VIKUNDI VYA KARETI WAIBUA MKAKATI WA KUOKOA VIJANA WALIOKUMBWA NA DAWA ZA KULEVYA

POLISI MOROGORO, VIKUNDI VYA KARETI WAIBUA MKAKATI WA KUOKOA VIJANA WALIOKUMBWA NA DAWA ZA KULEVYA

 

*Na Lilian Kasenene, Morogoro*

Matukio DaimaApp


JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro, kupitia kitengo cha Polisi Jamii kwa kushirikiana na kikundi cha mazoezi ya kareti cha SAYDO KARATE, limeanzisha oparesheni maalum ya kuwafikia vijana wanaojihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya aina ya bangi mitaani, kwa lengo la kuwabadilisha na kuwa sehemu ya jamii yenye tija.


Kuanzia Januari mwaka huu, vijana hao wamekuwa wakikusanywa na kupewa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya pamoja na mafunzo ya stadi za maisha. Baada ya hapo, wameunganishwa katika vikundi vya ujasiriamali ili kuwapatia njia mbadala ya kujipatia kipato halali na kuachana na vitendo vya uhalifu.


Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Morogoro, ACP Samwel Kijanga, amesema kuwa mabadiliko ya kifikra, mtazamo na matendo kwa vijana hao yamechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.


Kwa upande wake, Katibu wa Saydo Karate, Joseph Msimbe, amesema wazo hilo lilitokana na kuona fursa ya kutumia ujuzi wa kareti kama njia ya kuwavuta vijana na kuwajengea nidhamu.

“Hali hii ilituhamasisha kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kupata mafunzo maalum na kuanzisha rasmi mpango huu wa uokozi wa kijamii,” amesema.


Baadhi ya vijana walionufaika na mpango huo wameeleza kuwa sababu kuu ya wao kuingia katika biashara ya dawa za kulevya ilikuwa ni ugumu wa maisha.

Mmoja wa vijana hao, Ally Husein, ameishukuru juhudi hizo na kuomba jamii pamoja na wadau mbalimbali kuendelea kuwasaidia kwa kuwapatia fursa za ajira na mitaji ili waweze kuendeleza maisha yao kwa njia halali.

“Tumeanza kubadilika na tumetambua kuwa shughuli hizi si salama kwetu, hivyo tayari tumejirekebisha,” amesema.





Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3