MAKONDA: MSHINDI MISS WORLD TANZANIA KUIWAKILISHA TANZANIA KIMATAIFA
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
MSHINDI wa mashindano ya Miss World Tanzania 2026 anatarajiwa kupewa jukumu la kuiwakilisha Tanzania kimataifa kwa kupeperusha bendera ya taifa na kulinda heshima ya nchi katika jukwaa la dunia.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 13, 2026, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema mshindi huyo atakayepatikana Aprili 19 atabeba pia utamaduni na maadili ya Kitanzania.
Ameeleza kuwa mshiriki huyo atawakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia yatakayofanyika mwezi Septemba 2026 nchini Vietnam
Makonda amesema Tanzania imekuwa na historia ya kushiriki mashindano hayo mara 29, na mwaka huu mrembo mmoja kati ya 20 atachaguliwa kuiwakilisha nchi.
Aidha, amewahimiza washiriki wote kupambana kufikia ndoto zao na kutokata tamaa, akisisitiza kuwa kila mmoja ana kusudi lake maishani.
"Mashindano hayo ni fursa ya kuitangaza lugha ya Kiswahili kimataifa, akiwataka washiriki kuitumia kwa fahari wanapokuwa nje ya nchi, "Amesema Waziri Makonda
Kuhusu michezo, amesema maandalizi ya AFCON 2027 yanaendelea vizuri huku timu za taifa zikiendelea na mazoezi kama ilivyopangwa.
Amesisitiza kuwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan tayari imetoa fedha zote za maandalizi, hivyo hakuna kitakachokwama.
Pia amewataka wananchi kupuuza taarifa zisizo sahihi zinazosambaa mitandaoni kuhusu maendeleo ya sekta ya michezo.
Kwa upande mwingine, wizara imefungua milango kwa Watanzania wote wenye mawazo ya ubunifu kujitokeza ili kuwasilisha miradi yao na kupata ushirikiano wa serikali.
Mwisho


