Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MADEREVA WA SERIKALI WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI

MADEREVA WA SERIKALI WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI

 

Na Anold Deogratias Matukio Daima Media Kagera

Madereva wa serikali mkoani Kagera wametakiwa kuzingatia kikamilifu sheria za usalama barabarani, hususan kuepuka mwendo kasi, ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika na kulinda nguvu kazi ya taifa.


Wito huo umetolewa na kaimu Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Kagera, Yudi Kajange, katika mkutano mkuu wa chama cha madereva wa serikali (CMST) mkoa wa Kagera, ambapo ameleeza kuwa mwendo kasi kwa madereva wa serikali imekuwa ndio chanzo kikubwa cha kusababisha ajali barabarani.

“ukiangalia ajali nyingi za viongozi sababu ni mwendo kasi, unakimbia kwanini unaenda wapi bosi wako akikwambia twende tukimbie wewe ndiyo dereva ukipata ajali anayekuwa anahojiwa ni wewe, endesha kulingana na mwendo wako unaotakiwa kuendesha”

Awali akizungumza mwenyekiti wa CMST mkoa wa Kagera Ashirafu Kazinja amesema kuwa sababu inayopelekea madereva wa serikali kuendesha kwa kasi ni baadhi ya viongozi kutowaandaa mapema na safari madereva na kuanza safari kwa kuchelewa hivyo kuwalazimu madereva kuendesha kwa kasi ili kuendana na muda.

“tulifanya utafiti wa kujua mwendo kasi wa madereva wa serikali unasababishwa na nini tukagundua kwamba chanzo ni viongozi walio wengi kutotoa taarifa za safari mapema kwa madereva na kuanza safari kwa muda muafaka, unakuta bosi ana safari saa 12 jioni ya kwenda Dodoma lakini anakuja kumpa taarifa dereva saa sita kwamba kesho nina kikao”

Aidha katibu wa chama hicho mkoan wa Kagera Charles Buberwa amesema kuwa madereva wa serikali wanakabiliwa na changamoto kutopewa posho za ziada pale wanapopatiwa safari na kufanya kazi nje ya muda wa kazi hali inayowapelekea kutotekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“hawalipwi posho za ziada baada ya muda wa kawaida inayolingana na muda waliofanya kazi pili baadhi ya waajiri madereva wanaposafiri kikazi mikoa ya nje au kutoka wilayani na kuja mkoani na siku zikiongezeka wanaporudi hawalipwi posho waliyoahidiwa kulipwa kabla ya safari”

Kwa upande wake katibu tawala mkoa wa Kagera Stephen Ndaki aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo amewataka madereva hao kutunza magari yao, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kutunza siri za serikali.


“niwasisitize kutunza magari unajua hiyo ndio ofisi yako itunze kwa kuifanyia ukaguzi, lakini pia niwasisitize kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kutunza siri za serikali pale unapomsikia bosi wako anazungumza”

Pia katibu tawala huyo amewaahidi madereva hao kujenga au kuwatengea eneo maalum la kupumzikia madereva katika ofisi za halmashauri na ofisi za makao makuu ya mkoa.

Mkutano wa chama cha madereva wa serikali CMST ufanyika kila mwaka kwa lengo la kujadili na kuwasilisha changamoto zinazowakabili madereva wa serikali.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3