Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
HOFU YAZUKA MOROGORO BAADA YA KEMIKALI KUMWAGIKA KANDO YA BWAWA LA MINDU

HOFU YAZUKA MOROGORO BAADA YA KEMIKALI KUMWAGIKA KANDO YA BWAWA LA MINDU

 






Na Matukio Daima, Morogoro

Ajali iliyohusisha Lori la kubeba kemikali ya sumu aina ya sulphur imetokea katika barabara kuu ya Morogoro–Iringa na kuacha taharuki kubwa katika eneo la Bwawa la Mindu, baada ya kemikali hiyo kumwagika kwa wingi pande zote mbili za barabara huku upande wa Bwawa la Mindu Hali ikiwa mbaya zaidi.

Ajali hiyo imehusisha lori aina ya Howo lenye namba za usajili T 196 EMU likikokota tela namba T 243 ENS mali ya kampuni ya Alhushum ambalo dereva wake aliacha njia na kuparamia miti Kisha kuingia porini.


Hali hiyo ilisababisha kemikali iliyokuwa inasafirishwa kumwagika ardhini pande zote mbili za barabara.

Hofu imeubuka miongoni mwa wananchi kutokana na ajali hiyo kutokea katika eneo nyeti la karibu na Bwawa la Mindu, ambalo ni chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa Morogoro na kuzua wasiwasi mkubwa kuhusu athari za moja kwa moja kwa mazingira na usalama wa maji ya matumizi ya binadamu.

Mara baada ya tukio hilo kutokea, mamlaka mbalimbali zilifika eneo la tukio, zikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Bonde la Wami–Ruvu, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ingawa wamekataa kuzungumza lolote kwa madai kama timu Bado wanafanya uokozi na kuhakikisha mazingira yanakuwa salama.

Hata hivyo licha ya hatari ya Kemikali hiyo, watu waliokutwa wakiondoa Kemikali hiyo wengi wao walikuwa hawana vifaa vya kujikinga na hatari ikiwemo barakoa na kinga mikono (gloves)

Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali – Kanda ya Kati walipotafutwa wameahidi kutoa ushirikiano pindi wakifika Morogoro kwani walikuwa njiani kutokea Makao makuu ya Kanda Mkoani Dodoma.

Juhudi za kuzuia kemikali hiyo isiingie katika mifereji ya maji yanayoelekea Bwawa la Mindu sambamba na kuondoa kabisa Kemikali hiyo katika eneo la Ajali zimeonekana kuendelea hasa Majira ya usiku ambapo mtambo maalum ulifika kwa Kazi hiyo ili kusaidia uokoaji ambao awali ulionekana kufanywa watu wachache kwa mikono.

Hatari inaweza kujitokeza endapo kemikali hiyo itaingia kwenye mfumo wa maji au kama mvua ikinyesha katika eneo hilo.


Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3