WANYABIASHARA WA SOKO LA MKUYUNI WAOMBA MSAADA KWA SERIKALI BAADA YA MAAFA YA MVUA KUTOKEA.
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Wafanyabiashara wa Soko la Mkuyuni Jijini Mwanza wameiomba serikali kuwasaidia kutokana na bidhaa zao za biashara na nyumba kusombwa na maji kufuatia mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni na kusababisha mafuriko.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wafanyabiashara katika soko la Mkuyuni, wenye maduka na nyumba za kuishi walisema mvua hizo zimesababisha nafaka zao kulowana na hivyo kuharibika hivyo kuomba serikali kuwasaidia waweze kuendelea na shughuli zao hizo.
Katibu wa Soko la Mkuyuni, Simoni Mashamba alisema eneo hilo lina wafanyabiashara 300 na amekuwa akifanya biashara zake kwa zaidi ya miaka 30 kwenye soko hilo huku nyakati za mvua maji yalikuwa yakiingia sokoni lakini haijawahi kutokea maji kuwa mengi kiasi hicho.
Aliomba serikali iwasaidie kwani hasara waliopata ni kubwa hivyo imekata mitaji yao ya uendeshaji wa biashara kwani nafaka walizokuwa wanauza zimesombwa na maji na kuharibika.
Mfanyabiashara katika soko hilo anayejishughulisha na uuzaji wa nafaka, Emmanuel Madilisha alisema maji yalioingia katika soko hilo yalizidi kiwango hivyo udaga, mtama, mchele na uwele aliokuwa akiuuza umeharibika pamoja na kufanya jitihada za kukausha lakini hauwezi kutumiwa kwa matumizi ya binadamu.
Alisema vyakula hivyo vimeoza na kuchanganyikana na maji, taka vilevile udongo hivyo kuharibika kabisa haviwezi tena kuuzwa kwa matumizi ya chakula hivyo aliomba serikali iwasaidie kukabiliana na hasara hiyo iliyowakumba.
"Ona huu mchele, uwele umeanza kuota, unanuka huku ukiwa umeharibika haufai tena na udaga ukiwa unanuka sijui nifanyeje nimepata hasara kubwa" alilalamika Madilisha kwa huzuni kubwa.
Mfanyabiashara mwingine katika soko hilo, Leocardia Masaho alisema mchele wake umeenda na maji huku uliobaki ukiwa haufai tena kwa matumizi ya chakula hivyo kupata hasara kubwa.
Alisema ujenzi wa reli ya mwendokasi (SGR) umesababisha kuchimbwa kwa ardhi kiasi Cha kufanya kuwepo na eneo moja ambalo maji ya mvua kupita hivyo kumiminika kuja katika soko lao.
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo, Richard Masesa alisema walifika mapema katika eneo hilo ambapo waliweza kuokoa baadhi ya watu waliokuwa wamepanda juu ya paa za nyumba kuokoa maisha yao.
Alisema wananchi wamekumbwa na adha ya nyumba zao kubomoka huku wafanyabiashara wa nafaka wengi wao nafaka walizokuwa wakiuuza kuharibika.
Diwani huyo alisema kwa sasa serikali inafanya tathimini kuweza kufahamu madhara ya hasara iliyopatikana katika eneo hilo kutokana na mvua hiyo iliyonyesha.
Vilevile alisema serikali ina mpango wa kujenga soko katika eneo hilo hivyo anaamini tatizo lilowakumba wafanyabiashara litaisha kwa kupatikana kwa soko litalojengwa.


