WAKULIMA WA UYOGA WAIOMBA SERIKALI KUBORESHA MASOKO
Na Farida Mangube Morogoro
Wakulima wa uyoga mwitu kutoka mikoa mbalimbali nchini wameiomba serikali kuboresha upatikanaji wa masoko ya zao hilo pamoja na kudhibiti wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye maeneo yao ya uvunaji na kuharibu mazingira yanayochochea ukuaji wa uyoga.
Wakulima hao kutoka mikoa ya Tabora na Katavi wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kuuza uyoga kutokana na kukosekana kwa masoko ya moja kwa moja ya uhakika.
Aidha wamesema baadhi yao hulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta uyoga mwitu baada ya maeneo ya jirani kuvamiwa na wafugaji wanaoingiza mifugo yao na kuharibu ikolojia inayochochea ukuaji wa uyoga.
Mkulima wa uyoga kutoka Ilunde mkoani Katavi, Neema Maganga, amesema changamoto ya masoko imekuwa ikiwakatisha tamaa baadhi ya wakulima licha ya zao hilo kuwa na faida kubwa kiuchumi na kiafya.
Kwa upande wake mkulima kutoka mkoani Tabora, Catherine Chang’oma, amesema uvamizi wa mifugo katika maeneo ya misitu na mashamba umeathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa uyoga mwitu hali inayowalazimu wakulima kusafiri umbali mrefu kuutafuta.
Kutokana na changamoto hizo, Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Association for Development of Protected Area (ADAP) pamoja na vyuo vikuu kadhaa wameanzisha Jukwaa la Wadau wa Uyoga Tanzania lenye lengo la kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dk. Revocatus Mushumbusi, amesema jukwaa hilo linalenga kuja na tafiti mbalimbali zitakazosaidia kuboresha uvunaji, ukaushaji na upatikanaji wa masoko ya uyoga ili kuongeza thamani ya zao hilo.
Amesema maboresho hayo pia yatachangia kuboresha lishe kwa Watanzania kutokana na virutubisho vinavyopatikana kwenye uyoga.
Kwa upande wake Meneja Miradi wa ADAP, Romanus Mwakimata, amesema uyoga una uwezo mkubwa wa kutoa ajira hasa kwa wanawake na vijana endapo utawekewa mazingira bora ya uzalishaji na masoko.
Naye Mkurugenzi wa Utafiti wa Misitu kutoka TAFORI, Dk. Chelestino Balama, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha tafiti na elimu vinawafikia wakulima ili kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la uyoga.
Wadau hao wameeleza kuwa ushirikiano kati ya serikali, taasisi za utafiti na wakulima ni muhimu katika kuhakikisha zao la uyoga linakuwa chanzo kikubwa cha kipato na ajira kwa wananchi.




