MAFURIKO YAWAKOSESHA MAKAZI WANANCHI KILOSA
Na Matukio Daima,Kilosa
Wananchi kwenye kaya zaidi ya 118 katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wameathirika na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa nyumba pamoja na mali za wananchi, hali iliyowalazimu baadhi yao kuhama makazi yao kwa muda na kwenda kuishi kwa ndugu au katika maeneo mengine salama wakisubiri hatua za Serikali.
Mbali na athari hizo, mvua hizo pia zimeharibu miundombinu ya usafiri baada ya madaraja matatu kuathirika katika barabara ya Mikumi–Ruaha inayounganisha wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi, hali iliyosababisha usumbufu kwa wasafiri na wafanyabiashara.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amesema Serikali imeanza kufanya tathmini ya kina ya uharibifu uliotokea ili kubaini kiwango cha madhara pamoja na namna bora ya kuwasaidia wananchi waliokumbwa na maafa hayo.
Ameeleza kuwa daraja la Kidoma lililopo katika Kata ya Mikumi likikatiza mto Ruhembe , ni miongoni mwa miundombinu iliyoathirika vibaya na mvua hizo, jambo lililosababisha changamoto kubwa katika shughuli za usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.
Baadhi ya wananchi wanaotumia barabara hiyo wamesema uharibifu wa daraja hilo umeongeza muda wa safari na kuathiri shughuli za biashara kutokana na kulazimika kutumia njia mbadala.
Wananchi hao wameiomba Serikali kuharakisha ukarabati wa miundombinu iliyoharibika pamoja na kuwapatia msaada wale waliopoteza makazi na mali zao ili waweze kurejea katika maisha yao ya kawaida.




