Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TANZANIA YABADILI MWELEKEO PARACHICHI SASA KUPATA SOKO LA NDANI NA NJE KWA UBORA ULIOIMARISHWA

TANZANIA YABADILI MWELEKEO PARACHICHI SASA KUPATA SOKO LA NDANI NA NJE KWA UBORA ULIOIMARISHWA

 

Na Hamida Ramadan,Matukio Daima Media Dodoma

KWA muda mrefu, Tanzania imekuwa ikijikita zaidi katika kuhakikisha ubora wa mazao yanayosafirishwa nje ya nchi huku soko la ndani likipata uangalizi mdogo katika masuala ya usalama wa chakula.

Hata hivyo, mwelekeo huo sasa umeanza kubadilika, kufuatia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali kuimarisha zao la parachichi kuanzia uzalishaji hadi masoko ya kimataifa.

Miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana ni Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kuwezesha usajili wa kampuni 16 za Kitanzania zitakazouza parachichi katika soko la China, hatua inayofungua fursa mpya kwa wakulima na wafanyabiashara wa zao hilo.

Akizungumza jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Joseph Ndunguru, amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya kilimo na kufungua masoko ya nje.

Amesema pamoja na kufungua masoko hayo, serikali imeongeza nguvu katika kuboresha uzalishaji wa parachichi kwa kusambaza viuatilifu aina ya Comber sulphate katika mikoa inayolima zao hilo kwa wingi.

 "Lengo ni kudhibiti magonjwa ya mimea, hususan mnyauko wa majani, pamoja na kuimarisha ubora wa ganda la tunda hilo.

Katika hatua nyingine, TPHPA imeanza pia kufuatilia masalia ya viuatilifu kwenye mazao yanayotumiwa ndani ya nchi, tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo mkazo ulikuwa zaidi kwenye mazao ya kuuza nje, " Amesema. 

Mpango huo tayari umeanza katika mikoa 10 ya Tanzania Bara na unatarajiwa kupanuliwa hadi visiwa vya Unguja na Pemba.

Sambamba na hilo, zaidi ya mbegu elfu kumi zimehifadhiwa pamoja na sampuli za mimea mbalimbali kwa ajili ya kulinda bianuai na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali za kilimo kwa muda mrefu.

Prof. Ndunguru amesisitiza kuwa juhudi hizo zinalenga kulinda afya ya mlaji, kuongeza ubora wa mazao, na kuinua kipato cha wakulima kwa kuwapatia fursa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Hatua hizi zinaashiria mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo nchini, huku zao la parachichi likiendelea kupewa kipaumbele kama moja ya mazao ya kimkakati yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3