SIRRO AAGIZA WAKANDARASI WALIOTELEKEZA MIRADI KUKAMATWA
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro ameagiza kuwakamatwa wakandarasi wa miradi miwili iliyokuwa ikitekelezwa mkoani humo kwa kukimbia na kuitelekeza miradi hiyo huku wakiwa wamechukua fedha ya serikali.
Sirro alisema hayo alipofanya ziara kutembelea miradi ya nyongeza inayotekelezwa kupitia mradi wa ujenzi wa kituo cha pamoja cha Forodha (OSBP) kinachojengwa katika eneo la Manyovu wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Mpakani na nchi ya Burundi.
Awali Balozi Sirro alitembelea Mradi wa nyongeza wa ukarabati wa hospitali ya wilaya Kasulu unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.3 uloanza Julai 31 mwaka 2024 ukitarajiwa kukamilika Julai 2025 lakini hadi sasa mradi umefikia silimia saba ya utekelezaji wake na Mkandarasi wa mradi huo M/s Gemini Engineering Co.Ltd amekimbia eneo la mradi tangu mwaka jana.
Kaimu Meneja wa Wakala wa barabara mkoa Kigoma, Mhandisi Chora Kimata akitoa maelezo wa Mkuu wa mkoa Kigoma alisema kuwa Mkandarasi huyo tayari ameshalipwa malipo ya awali kiasi cha shilingi milioni 208.2 ambapo kutokana na Mkandarasi huyo kutokuwepo eneo la kazi wamevunja mkataba huyo.
Katika mradi wa pili Mkuu huyo wa mkoa alishuhudia kukwama kwa mradi wa maji safi na maji taka mji wa Kasulu wilaya ya Kasulu wenye thamani ya shilingi Bilioni 2.2 ambapo Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa Kigoma Charo Kimata alisema kuwa Mkandarasi kampuni ya M/S KGG Investimate Limited tayari ameshalipwa kiasi cha shilingi Bilioni 1.3 na utekelezaji umefikia asilimia 60 huku fedha iliyolipwa ni Zaidi ya asilimia 59.
Kaimu Meneja wa Wakala wa barabara mkoa Kigoma, Chora Kimata alisema kuwa jumla ya miradi 12 ya nyongeza inatekelezwa kupitia mradi mkubwa wa ujenzi wa forodha ya pamoja katika eneo la Manyovu wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Mpakani na nchii ya Burundi ambapo kiasi cha shilingi Bilioni 34 zinatarajia kutumika kwa mradi huo.
Akihitimisha ziara hiyo Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa pamoja na kukamatwa kwa wakandarasi hao amezitaka kamati za ulinzi na usalama za wilaya kufanya za mara kwa mara kwenye miradi ili kubaini mapema changamoto zilizopo
Mwisho.



