RC LINDI - AHAMASISHA KUENDELEZA MEMA BAADA YA MFUNGO
Hadija Omary
Lindi – Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zainab Tellack, amewahasa waumini wa dini ya Kiislamu na Kikristo kuendeleza mema yote waliyokuwa wakiyafanya wakati wa kipindi cha Ramadhani na Kwaresma, ikiwemo kukemea na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Bi. Tellack ametoa wito huo wakati wa futari ya pamoja iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi, iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa mkoa huo.
Amesema kuwa baada ya waumini wa Kiislamu kumaliza mwezi mtukufu wa Ramadhani na Wakristo kukamilisha mfungo wa Kwaresma, wanapaswa kuendelea kutenda mema na kuzingatia maadili mema waliyojifunza katika kipindi hicho cha ibada.
“Ni muhimu kwa kila mmoja kujitafakari kama ataendelea na mwenendo mzuri aliouanza wakati wa mfungo au atarejea katika matendo ya awali yasiyofaa,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi, Emma Mwasyenge, amesema kuwa pamoja na kuandaa futari hiyo, taasisi hiyo pia imetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wanaoishi katika kituo cha Loving and Heart, ikiwa ni sehemu ya kuonyesha kujali jamii.
Baadhi ya wadau walioshiriki katika futari hiyo wameipongeza TAKUKURU kwa kuandaa tukio hilo, wakisema kuwa limeimarisha imani yao kwa taasisi hiyo na kuongeza mshikamano miongoni mwa wadau.
.jpeg)

.jpeg)