Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MBUNGE MLIMBA AWATEMBELEA MABINTI 300 FDC IFAKARA, AWAPATIA MAHITAJI YA MASOMO

MBUNGE MLIMBA AWATEMBELEA MABINTI 300 FDC IFAKARA, AWAPATIA MAHITAJI YA MASOMO

 


Mbunge wa Jimbo la Mlimba, KellenRose Rwakatare, ametembelea mabinti zaidi ya 300 wanaosoma katika Chuo cha Maendeleo FDC Ifakara na kuwapatia mahitaji mbalimbali muhimu yatakayowawezesha kuendelea na masomo yao ya ufundi stadi kwa ufanisi.

Ziara hiyo iliyofanyika katika mji wa Ifakara imelenga kuwatia moyo wanafunzi hao wa kike, kuwasikiliza changamoto wanazokutana nazo katika safari yao ya elimu, pamoja na kuthibitisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwawezesha vijana wa kike kielimu na kiuchumi.

Akizungumza na wanafunzi hao wakati wa ziara hiyo, Mbunge Rwakatare alisema kuwa serikali chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele katika kuwainua wanawake na vijana kwa kuwapatia fursa za elimu na ujuzi zitakazowawezesha kujitegemea katika maisha yao.


“Serikali inaamini kuwa msichana akipewa elimu na ujuzi, si tu anajiendeleza yeye binafsi bali pia anaijenga familia yake na jamii kwa ujumla. Ninyi ni matumaini ya taifa letu, hivyo tumieni vizuri fursa hii mliyoipata,” alisema Mbunge Rwakatare.

Katika ziara hiyo, Mbunge huyo alikabidhi vifaa na mahitaji mbalimbali ya kujifunzia ambayo yanatarajiwa kuwasaidia wanafunzi hao katika kuendeleza masomo yao ya ufundi stadi katika fani mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo.

Mbunge huyo pia aliwahimiza mabinti hao kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu katika masomo yao na kutumia vyema ujuzi wanaoupata ili baadaye waweze kujiajiri au kuajiriwa na kuchangia maendeleo ya taifa.

Aidha, alisisitiza kuwa vijana wa kike wanapaswa kuwa na ujasiri wa kufikia ndoto zao na kuepuka vitendo vinavyoweza kuharibu mustakabali wao kama vile kuacha masomo au kujiingiza katika mienendo isiyofaa.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho walieleza kufurahishwa na ziara hiyo wakisema imewapa hamasa kubwa ya kuendelea kusoma kwa bidii. Walisema msaada waliopokea utawasaidia kukabiliana na baadhi ya changamoto walizokuwa wanakutana nazo katika masomo yao.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3