JAMII YAHIMIZWA KUSHIRIKIANA NA TAKUKURU KUPAMBANA NA RUSHWA NA KUIMARISHA UWAJIBIKAJI MBEYA
Na, Samwel Mpogole: Mbeya.
Jamii imetakiwa kushirikiana kwa karibu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika juhudi za kudhibiti vitendo vya rushwa na kuimarisha uwajibikaji, ikiwa ni hatua muhimu katika kulinda maendeleo ya taifa.
Wito huo umetolewa na Jasper Luoga Naibu TAKUKURU Mkoa wa Mbeya wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na taasisi hiyo kwa wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani humo.
Amesema kuwa ushirikiano wa wananchi ni nguzo muhimu katika kufichua na kuzuia vitendo vya rushwa vinavyoweza kudhoofisha ustawi wa jamii na uchumi wa nchi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya, Mohamed Fakili Azizi, amesisitiza umuhimu wa mshikamano miongoni mwa wananchi.
Amewataka wakazi wa Mbeya kuungana kwa pamoja kupinga vitendo vya uovu vinavyohatarisha maadili na maendeleo ya mkoa huo.
Kwa upande wao, wadau waliohudhuria hafla hiyo, akiwemo Mwenyekiti wa Jumuia ya Maridhiano Mkoa wa Mbeya, Askofu Oscar Ongere, wameeleza kuwa elimu inayotolewa na TAKUKURU imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu athari za rushwa.
Wameahidi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo pamoja na kuendeleza umoja na mshikamano katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo.
Hafla hiyo ya futari imelenga kuimarisha uhusiano kati ya TAKUKURU na wadau wake, sambamba na kujadili mikakati madhubuti ya kuendeleza vita dhidi ya rushwa, kwa lengo la kujenga jamii yenye uadilifu, uwajibikaji na maendeleo endelevu.

