WANUFAIKA MIKOPO ASILIMIA 10 WATAKA VIKWAZO KUPUNGUA ZAIDI.
Feb 13, 2026
Na Moses Ng’wat, MBOZI.
WANUFAIKA wa mikopo ya asilimia 10 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi wamewaomba maafisa maendeleo ya jamii kuwasaidia kuboresha taarifa zao wakati wa uombaji wa mikopo hiyo, ili waweze kuipata kwa wakati na kuepuka kupishana na fursa za kibiashara zinazojitokeza kwa wakati husika.
Wakizungumza katika hafla ya kukabidhiwa mikopo hiyo, Februari 13, 2026 na kufanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Wilaya, wamesema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni kurejeshewa mara kwa mara fomu zao kwa ajili ya marekebisho, jambo linalochelewesha mchakato na kuwakatisha tamaa wengi wao.
Mmoja wa wanufaika hao, Prisca Mwashitete, alisema endapo ujazaji wa fomu na maandalizi ya nyaraka utafanyika kwa ushirikiano wa karibu kati ya vikundi vya wanufaika na Maafisa Maendeleo ya Jamii, itasaidia kupunguza makosa yanayojitokeza na kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa mikopo hiyo.
Amebainisha kuwa kuchelewa kukamilika kwa taratibu kunawafanya washindwe kutumia fursa za kibiashara zinazohitaji mtaji wa haraka, hususan katika sekta za kilimo, biashara ndogo ndogo na ufugaji.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Danny Tweve, katika awamu ya pili halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 689, ambapo vikundi vya wanawake vimepata Sh milioni 276, vijana Sh milioni 384.6 na watu wenye ulemavu Sh milioni 28.4.
Akihutubia katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, amesisitiza kurejeshwa kwa wakati kwa mikopo hiyo na kuwataka wanufaika kuepuka kuitumia katika matumizi yasiyo ya kibiashara.
Ameonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya vikundi au wanufaika watakaoshindwa kufanya marejesho kwa mujibu wa makubaliano, ili kuhakikisha fedha hizo zinaendelea kuwanufaisha wananchi wengine.



