Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.

WADAU wa Kilimo katika sekta ndogo ya Pamba nchini, wameiomba serikali kuwapatia ruzuku itakayosadia kuendesha shughuli za kilimo pia itamwongezea mkulima uzalishaji na kukuza matumizi ya Teknolojia kwa lengo la kuongeza tija, kukuza Uchumi na pato la Taifa.


Aidha wadau hao wamewaomba baadhi ya wanasiasa kuunga mkono Teknolojia mbalimbali zinazoletwa na serikali kwa wakulima ili kumwongeze tija mkulima ikiwemo Matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones), Maboza (Boom Spray) pamoja na Maafisa Ugani kupitia Mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT).


Hayo yamebainishwa juzi na Katibu Chama cha Wanunuzi wa Pamba Tanzania (TCA), Boaz Ogolla wakati akiongea na waandishi wa Habari za Pamba, ambapo akisisitiza Ruzuku inahitajika kwenye sekta ya Pamba kutokana na kushamiri kwa matumizi ya Teknolojia.

Katibu Chama cha Wanunuzi wa Pamba Tanzania (TCA), Boaz Ogolla wakati akiongea na waandishi wa Habari za Pamba (hawapo pichani) kuhusu uzalishaji wa Pamba.


Alisema kuwa wakulima wa Pamba nchini, wameshatoka kwenye matumizi ya jembe la mkono na kuingia kwenye Teknolojia kwa lengo la kuwaongeza tija,watoke kuzalishaji kutoka kilo 300 na kufikia kilo 800 mpaka 1,000 kwa ekari moja.



"Ruzuku inahitajika kwenye sekta ya Pamba, wakulima na Wadau wa Pamba tumetoka kwenye jembe la mkono na kuanza matumizi ya Teknolojia, kuna Matrekta, Maboza, ndege nyuki kwa lengo la kumrahisishia mkulima shughuli za kilimo...Kama Kuna nafasi ya ruzuku watuletee ili tuzalishe Kwa tija" amesema Ogolla.


Amesema Mkulima wa Pamba bado anapata tija ndogo, hivyo anatakiwa kuendelea kupewa Elimu juu ya matumizi sahihi ya Teknolojia ikiwemo Matumizi ya mbolea pamoja na kupima Afya ya udongo.


Amefafanua kuwa tija ya BBT kwa sasa haiwezi kuonekana lakini baada ya miaka miwili au Mitatu wakulima watakuwa wameshaanza kubadilika na kuweza kutumia Elimu ya ugani kuhudumia mashamba yao.

Wakulima wa Pamba Kijiji Cha Budalabujiga wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu wakipata maelekezo juu ya matumizi ya ndege isiyo ya rubani ambayo imetolewa na serikali kwa ajili ya upiliziaji wa Pamba.


" Lengo letu ni kuongeza tija, kumpa Elimu mkulima kupitia BBT ili aongeze uzalishaji, wanaopinga BBT wanahitaji elimu...kuna wakulima wanalima na kupata kilo 200 au 300, Kilichopo ni kuongeza tija kwa kumpa Elimu mkulima, wataalamu wamfundishe mkulima kuongeza tija." Amesema 

Trekta likipulizia dawa shambani.


Katika hatua nyingine, Ogolla ambaye pia ni Meneja wa Kiwanda cha Alliance Ginneries ameipongeza Bodi ya Pamba (TCB) kwa kusambaza pembejeo za dawa kwa wakati ili kumrahisishia mkulima shughuli za kilimo.


Amesema wakulima wanaendelea kuelimishiwa juu ya Matumizi ya molasisi kudhibiti wadudu ambapo Majukumu ya Wanunuzi wa Pamba kipindi hiki ni kufikishia.


"Kugawa dawa kidigitali imesaidia Kuimarisha na kujua ukubwa na idadi ya mashamba, itasaidia kupunguza matumizi mabaya ya dawa na kujua idadi ya ekari zilizopo vijijini...BBT wanachukua takwimu sahihi za wakulima na hakuna mkulima anayelaalamikia dawa" amesema Ogolla.

Maboza yaliyotolewa na serikali kwa ajili ya shughuli ya upiliziaji.


Paul Robert mkulima na mkazi wa Kijiji cha Nyamswa aliipongeza serikali kujikita kwenye matumizi ya Teknolojia ili kumrahisishia mkulima kutekeleza shughuli za kilimo pia zimepunguza muda wa kushinda shambani.


Mwisho.

Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Maswa, Ally Mabrouk akiwafundisha wakulima juu ya matumizi ya drone kwenye mashamba yao.
Ndege nyuki ikipulizia dawa mashambani.


Mkulima wa Pamba akipulizia Pamba shambani.