Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
VETA YAZINDUA MPANGO WA USHIRIKIANO KATI YA VYUO NA VIWANDA NA KUFADHILI WANAfunzi WENYE ULEMAVU

VETA YAZINDUA MPANGO WA USHIRIKIANO KATI YA VYUO NA VIWANDA NA KUFADHILI WANAfunzi WENYE ULEMAVU

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa VETA, CPA Anthony Mzee Kasore, amesema Serikali imeandaa Mpango wa Kitaifa wa Ushirikiano kati ya vyuo na viwanda uliozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Daktari Emmanuel Nchimbi, tarehe 9 Februari 2026.

CPA Kasore amesema mpango huo unatekeleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuunganisha elimu ya ufundi na ajira, hivyo kuhakikisha vijana wanaweza kupata ajira au kujiingizia kipato kwa kushirikiana na viwanda.

“Kwa mwelekeo huu, mpango wa Rais wa kuunganisha viwanda na vyuo vya mafunzo unajidhihirisha vyema,” amesema.

Amesema VETA pia imefanya tafiti 13 za soko la ajira, ikiwemo uchambuzi wa mahitaji ya ujuzi (Skills Mapping) katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini, ili kuandaa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya kiuchumi ya kila eneo.

Mkurugenzi huyo ameeleza mafanikio ya siku 100 za Rais Samia, akisema VETA imejipanga kuwafikia mafundi waliopo mitaani na katika maeneo ya kazi ili kuwapima na kuwatunuku vyeti kupitia mpango wa Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (RPL). 

Hadi Januari 2026, jumla ya wanagenzi 25,523 (wanaume 21,547 na wanawake 3,976) wamenufaika na mpango huo, huku VETA ikilenga kurasimisha mafundi 30,000 katika mwaka wa fedha 2025/2026. Lengo ni kufikia vijana 80,000 ifikapo Juni 2027.

“Kwa mafundi wengi wanaofanya kazi kwa ufanisi lakini hawana vyeti rasmi, VETA tutawafuata ili kuwarasimisha na kuwapatia vyeti vitakavyowawezesha kupata ajira na zabuni,” amesema CPA Kasore.



Mbali na urasimishaji ujuzi, VETA inatekeleza Mpango wa Mafunzo Jumuishi ya Kukuza Ujasiriamali kwenye Sekta Isiyo Rasmi (INTEP), ambao unalenga kuongeza ujuzi kwa vijana na wanawake wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi zisizo rasmi kama vile mama na baba lishe, mafundi nguo, seremala na wasindikaji. 


Amesema hadi Januari 2026, jumla ya wajasiriamali 7,040 wamenufaika, huku VETA ikipanga kuwafundisha vijana na wanawake 2,000 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.


Aidha, VETA imeanzisha mfumo wa VSOMO, ambao unawawezesha wanafunzi kujifunza mafunzo ya ufundi stadi kupitia simu za mkononi, kufanya mitihani ya nadharia, kisha kuendelea na mafunzo ya vitendo chuoni. CPA Kasore amesema.



“Hii inapunguza muda wa kukaa chuoni, inaongeza matumizi bora ya simu za mkononi na inawapa fursa watu walio mbali na vyuo kupata mafunzo ya ufundi stadi.”


Aidha, mwaka huu, VETA itafadhili wanafunzi 195 wenye ulemavu waliodahiliwa katika mafunzo ya muda mrefu, ambapo ada zao zitatolewa kwa miaka yote ya mafunzo kuanzia ngazi ya kwanza hadi ya pili. 



Mkurugenzi huyo amewahimiza wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu kuwaleta kwenye vyuo vya VETA ili wapate ujuzi unaowawezesha kujikwamua kiuchumi na kimaisha.


Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3