VIJANA WAONYWA MATUMIZI YA DAWA ZA, KULEVYA
Na Matukio Daima Media ,Morogoro
Tasnia ya vijana imepata pigo kubwa kutokana na kuendelea kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kulevya, hali inayotajwa kuhatarisha mustakabali wa kizazi cha sasa na kijacho.
Waziri Nanauka akisikiliza kwa makini mada mbalimbali katika maadhimisho hayo
Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Vijana, Joel Nanauka, alisema tabia hiyo inaua vipaji, inapoteza nguvu kazi na kudhoofisha maendeleo ya taifa.
Alitoa kauli hiyo katika kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Portable Practical Education Preparation PPEP na kufanyika chuo Kikuu cha Jordan mjini Morogoro.
Nanauka alisema Afrika ya kesho inahitaji vijana waliotayari kimaadili, kielimu na kiafya.
Naye Dk Onesmo Nyinondi, mwakilishi wa Rais wa PPEP kwa upande wa Tanzania walioandaa Kongamano hilo kubwa kwa kushirikiana na vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi chini likiwa na kaulimbiu ya “Afrika ya Kesho" anayetokea chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, alisema mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji ushirikiano wa familia, Serikali, taasisi za elimu na jamii kwa ujumla.
Nao baadhi ya Wadau walisema bila kuchukua hatua sasa, taifa linaweza kupoteza kizazi muhimu cha viongozi wa baadaye.
Kamishna wa Tiba na Kinga wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Dk Peter Mfisi, akimwakilisha Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo,Aretas Lyimo, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mikakati ya kuzuia matumizi ya dawa hizo kwa kutoa elimu na kudhibiti biashara haramu.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Dk Adolf Makauki,kutoka chuo Kikuu Mzumbe amesema kongamano hilo linalenga kutafuta suluhisho endelevu la tatizo la dawa za kulevya kwa vijana.





