Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TUNDU LISSU ASHINDA MAPINGAMIZI YAKE

TUNDU LISSU ASHINDA MAPINGAMIZI YAKE

 

Na Matukio Daima Media

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imekubaliana na mapingamizi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mshtakiwa katika kesi ya uhaini, Tundu Lissu, kupinga uhalali wa notisi ya ushahidi wa ziada iliyowasilishwa na Jamhuri kupitia kwa shahidi wake, ACP Amini Mahamba.

Mahakama imesema notisi hiyo haikidhi matakwa ya Kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Jana, Februari 23, 2026, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, uliieleza mahakama kuwa uliwasilisha notisi hiyo kwa lengo la kuwasilisha ushahidi wa ziada kutoka kwa ACP Mahamba, aliyekuwa kiongozi wa upelelezi wa matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

 Upande wa mashtaka ulidai kuwa walibaini uwepo wa ushahidi huo wakati wakimuandaa shahidi huyo kutoa ushahidi wake Februari 16, 2026.

Akisoma uamuzi mdogo wa mahakama, Jaji Dunstan Ndunguru alisema mahakama imezipitia kwa kina hoja za pande zote mbili — za Jamhuri zilizojengwa chini ya Kifungu cha 308(1), (2), (3) na (4) cha CPA, na mapingamizi ya Lissu yaliyojengwa chini ya kifungu hicho hicho — na kujiridhisha kuwa notisi hiyo haikidhi vigezo vya kisheria.

“Ninaona kwamba kifungu hicho kinafungua mlango wa kuletwa ushahidi wa shahidi ambaye maelezo yake yalikuwepo lakini kwa bahati mbaya hayakusomwa wakati wa mwenendo wa ukabidhi (committal proceedings). 

Hata hivyo, hakifungui mlango wa kuleta ushahidi mpya ambao haukuwepo au haukuletwa, au ambao umepatikana baadaye baada ya mwenendo wa ukabidhi kukamilika,” alisema Jaji Ndunguru.

Mahakama ilifafanua kuwa kwa mujibu wa rekodi za mahakama na maelezo ya Jamhuri, ushahidi wa awali wa ACP Mahamba tayari ulisomwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati wa mwenendo wa ukabidhi. 

Hata hivyo, ushahidi ambao Jamhuri ilikusudia kuuongeza unahusu mambo yaliyopatikana wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, hivyo hauangukii katika wigo wa Kifungu cha 308 cha CPA.

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo mdogo, mahakama iliahirisha shauri kwa muda mfupi kufuatia ombi la upande wa Jamhuri kupewa nafasi ya kutafakari hatua za kuchukua.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3