MAKAMISHNA WALIOVISHWA VYEO TAWA WAHIMIZWA USHIRIKISHWAJI,UBUNIFU
Na Matukio Daima Media , Morogoro
MAKAMISHNA wapya wa Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori Tanzania TAWA waliovishwa vyeo vipya vya kijeshi wamehimizwa kutumia ubunifu na kushirikiana na watumishi walioko chini na juu yao kuboresha utendaji wa taasisi hiyo.
Kamishna Msaidizi wa uhifadhi wa TAWA Mlage Yusuph Kabange akizungumza na hadhira iliyofika makao makuu ya Mamlaka hiyo kushuhudia upandishwaji wa vyeo vya kijeshi makamishna 13 wa Mamlaka hiyo
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko amewavisha vyeo hivyo vya kijeshi Makamishna wa Uhifadhi (13) katika hafla ya Kijeshi iliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo, Mjini Morogoro.
Licha ya kuwapongeza kwa kuaminiwa na Bodi ya Wakurugenzi na kuteuliwa katika nafasi hizo katika maeneo mbalimbali ya usimamizi, akawaelekeza kutekeleza maelekezo ya Serikali na maono ya Bodi ya nne ya Wakurugenzi ya TAWA ya kuhakikisha mamlaka hiyo inapaa katika viwango vyote vya utendaji kazi ikiwemo ushirikishaji wa jamii, usimamizi wa kazi za uhifadhi, kuendeleza Utalii, kuongeza uwekezaji na ukusanyaji wa mapato.
Aidha Mwenyekiti huyo akawataka Makamishna wa uhifadhi kwenda kufanya kazi kwa kushirikiana na Maafisa na Askari walio chini yao kwa kuzingatia miongozo iliyopo huku wakizingatia ubunifu, weledi, sheria na utu.
Makamishna wa Uhifadhi waliovishwa vyeo ni pamoja na Makamishna Wasaidizi Waandamizi (7) ambao ni Privatus Kasisi, Wilbright Munuo, Khadija Malongo, Mark Chuwa, Vicky Kamata, Omary Msangi na Orest Njau.
Kwa upande wa Makamishna Wasaidizi ni Alphonce Mung’ong’o, Jackson Msaki, Suleiman Keraryo, Jovine Nachihangu, George Makheya na Rajabu Hochi.
Mapema Kaimu Kamishna wa Uhifadh
i wa TAWA, Mlage Yusuph Kabange na Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Rasilimali watu Thabiti Maarufu kwa nyakati tofauti walisema wanatarajia makamishna hao kuwa chachu ya kufanikisha maelekezo mbalimbali ya Serikali katika kuimarisha utoaji wa huduma za mamlaka hiyo
Wakasema makamishna hao kama wasimamizi wa wengine hawana budi kuzingatia Sheria, kanuni na miongozo na maelekezo yanayotolewa na Serikali,mamlaka na viongozi wa Taasisi na Wizara ili kuboresha utendaji kazi.
Aidha wakawasihi kuishi kwa ushirikiano na wananchi wanaozunguka hifadhi, viongozi wa kiserikali na kuibeba vyema dhamana ya kulinda rasilimali za Taifa.
" Mafanikio yenu yatapimwa kwa matokeo chanya katika uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za uhifadhi na wanyamapori" Aliongeza Kabange.





