TGNP YAWAJENGEA UWEZO WAFUGAJI KUDHIBITI MABADILIKO YA TABIA NCHI IRINGA
Schola Makwaia Mkufunzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)
Na Herieth Molla, Matukio Daima Media Iringa
Tanzania (TGNP) umetoa mafunzo kwa waelimishaji wa ngazi ya jamii katika halmashauri mbili za mkoa wa Iringa ambazo ni Iringa Vijijini na Kilolo, kwa lengo la kuwawezesha wanawake na vijana kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia kilimo na ufugaji wa kisasa unaotunza mazingira.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamejikita katika kuwaongezea washiriki uelewa kuhusu ufugaji wenye tija na kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Wanufaika wakuu wa mafunzo hayo ni wanawake na vijana wanaojishughulisha na ufugaji na kilimo katika jamii zao.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, mwezeshaji kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi Schola Makwaia, alisema mafunzo hayo yametolewa kupitia mradi wa Ustahimilivu Wake, Dunia Yetu (Her Resilience, Our Planet) unaolenga kuwajengea uwezo wanawake na vijana wanaojishughulisha na ufugaji ili waweze kutambua mabadiliko ya tabianchi, athari zake na namna ya kupunguza makali yake.
Bi Makwaia alieleza kuwa katika mkoa wa Iringa, mradi huo unatekelezwa katika wilaya za Kilolo, Iringa Vijijini na Mufindi, na kwamba matarajio ya TGNP ni kuwa waelimishaji waliopata mafunzo hayo watakuwa chachu ya mabadiliko katika jamii zao kwa kusaidia wafugaji wenzao pamoja na jamii inayowazunguka, kukabiliana na athari hizo.
Alibainisha kuwa mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakiwaathiri zaidi wanawake kwa kuwaongezea mzigo wa majukumu kama kutafuta maji na malisho ya mifugo yao kwa umbali mrefu, upungufu wa chakula na majukumu ya malezi, huku vijana wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira unaosababishwa na kuongezeka kwa gharama za kilimo na ufugaji.
Katika hatua nyingine, Bi Makwaia aliwataka waelimishaji hao kuhakikisha elimu waliyoipata inawafikia wafugaji na wakulima wengi zaidi ili kuongeza idadi ya waelimishaji ngazi ya jamii na kufanikisha juhudi za pamoja za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuongezeka nchini.
Mmoja wa washiriki vijana wa mafunzo hayo, Pascal Sichawel kutoka kijiji cha Mangalali, Kata ya Ulanda, tarafa ya Kalenga, alisema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa changamoto kubwa kwake, hususani ukosefu wa malisho na maji kwa mifugo pamoja na mvua chache na joto kali linaloharibu mazao.
“Ukame hasa kipindi cha kiangazi unatutesa sana maji na malisho yanakuwa adimu, na wakati mwingine tunalazimika kuchimba visima vifupi ambavyo havitoshelezi maji ukilinganisha na idadi ya mifugo tuliyonayo,” alisema Pascal.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa umuhimu wa kupunguza wingi wa mifugo isiyo na tija, kupanda na kuhifadhi malisho pamoja na kuachana na ufugaji holela na kutumia mbinu za kisasa za kilimo na ufugaji.
Naye Veronika Mgongolwa, mkazi wa kijiji cha Mangalali, alisema mabadiliko ya tabianchi yameathiri zaidi ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, lakini elimu aliyopata imemsaidia kujifunza mbinu za ulimaji, upandaji, uvunaji na uhifadhi wa malisho pamoja na uvunaji wa maji ya mvua kwa gharama nafuu.
“Elimu hii imenipa ujasiri wa kuwaelimisha wengine katika jamii yangu ili kwa pamoja tuweze kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Veronika.
Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Deodatha Kalinga, alisema mabadiliko ya tabianchi yameongeza mzigo wa kazi kwa wanawake na kuifanya shughuli za kilimo na ufugaji kuwa na gharama kubwa zaidi, hali inayowaathiri vijana wengi kushindwa kuendelea na shughuli hizo.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mifugo, kutoka wilaya ya Kilolo, Dkt. Mahenge Julius, alisema mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha usawa wa kijinsia katika jamii kwa kupunguza mzigo wa majukumu kwa wanawake na kuhimiza ushirikiano wa kifamilia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mradi wa Ustahimilivu Wake, Dunia Yetu (HROP) unafadhiliwa na Serikali ya Canada na unatekelezwa kwa kipindi cha miaka sita kuanzia Septemba 2024 hadi Machi 2030 katika vijiji 300 vya mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya. Mradi huo unatekelezwa na CARE Tanzania kwa kushirikiana na WWF Tanzania, SAGCOT Centre Ltd, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Shahidi wa Maji (SwM) na Conservation Farming Unit Tanzania (CFU–Tanzania).
.jpg)

