TAKUKURU MBEYA YAOKOA ZAIDI YA MILIONI 107 ZA POS, WANANCHI 20 WAREJESHEWA FEDHA.
Na: Samwel Mpogole
MBEYA -
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mbeya imeendelea kuonyesha makali yake katika mapambano dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma, baada ya kuokoa jumla ya shilingi 107,450,300 zilizokuwa hazijawasilishwa katika akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu taarifa ya utendaji ya kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Josper Luoga, amesema fedha hizo ni sehemu ya makusanyo ya POS yaliyofanywa na watoza ushuru, ambapo jumla ya shilingi 125,431,000 zilikusanywa lakini hazikuwasilishwa ipasavyo kwenye akaunti ya halmashauri.
Amesema kupitia uchunguzi wa kina uliofanywa na TAKUKURU, kiasi hicho kikubwa cha fedha kimeokolewa na hatua stahiki zimechukuliwa ili kuhakikisha wahusika wanawajibika kwa mujibu wa sheria.
“Lengo letu ni kulinda rasilimali za umma na kuhakikisha kila senti inayokusanywa inafika kwenye mifumo rasmi ya serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi,” alisisitiza Luoga.
Katika hatua nyingine, Tosha amesema kuwa TAKUKURU mkoa wa Mbeya imewezesha wananchi 20 wa Mtaa wa Tosha, Kata ya Ilomba, ndani ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya kurejeshewa jumla ya shilingi 500,000 walizokuwa wamechukuliwa kwa njia isiyo halali.
Ameeleza kuwa Fedha hizo zilikusanywa na mtu aliyetambulika kwa jina la Alex Nyagawa, ambaye ni mkandarasi binafsi na si mtumishi wa TANESCO. Inadaiwa kuwa aliwahadaa wananchi hao kwa kuwaahidi kuwaunganishia umeme wa REA kwa gharama ya shilingi 27,000 inayotolewa vijijini, huku kila mwananchi akitozwa shilingi 25,000.
Baada ya malalamiko kufikishwa TAKUKURU na kufanyiwa uchunguzi, fedha hizo zilirejeshwa kwa wahusika, hatua iliyopokelewa kwa faraja na wakazi wa eneo hilo.
TAKUKURU imetoa wito kwa wananchi kuwa makini dhidi ya watu wanaojifanya mawakala au watumishi wa taasisi za umma bila kuwa na mamlaka halali. Wananchi wametakiwa kuhakikisha wanathibitisha taarifa kupitia ofisi rasmi kabla ya kufanya malipo yoyote.
