RC MAKALLA AWATAKA WATENDAJI KATA KUWAJIBIKA IPASAVYO.
Na,Jusline Marco;Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla amezindua utaratibu wa usikilizaji kero na uwajibikaji kwa Watendaji wa Mitaa na Kata, huki akitangaza kuwa upimaji wa Viongozi hao katika utendaji utatokana na namna walivyotatua kero za wananchi katika maeneo yao.
CPA Makalla amezindua utaratibu huo Februari 27, 2026 wakati alipokutana na Viongozi na Watendajj wa Halmashauri za Wilaya za Arumeru na Arusha pamoja na Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya za Mkoa wa Arusha, ambapo amesema asilimia kubwa ya kero zipo kwenye sekta ya ardhi katika ngazi ya Vijiji na Kata.
Katika maelekezo yake CPA Makalla ameagiza kila Halmashauri kuwa na dawati la kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kila Afisa ardhi kutenga siku moja kwa kila wiki kwaajili ya kushughulikia kero za wananchi katika maeneo yao.
Amebainisha kuwa Ofisi yake na Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Arusha wataendesha Kliniki maalumu za usikilizaji na utatuzi wa kero za wananchi, ambapo amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuimarisha na kuyajengea uwezo Mabaraza ya ardhi kupitia mafunzo na semina mbalimbali pamoja na kusisitiza Mabaraza hayo kutenda haki katika kuwahudumia wananchi.


