Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
SERIKALI YAANZISHA MPANGO WA KUNUSURI ZAO LA MINAZI LINDI YAGAWA MICHE BURE

SERIKALI YAANZISHA MPANGO WA KUNUSURI ZAO LA MINAZI LINDI YAGAWA MICHE BURE

 


Na Matukio Daima Media, Lindi 

Kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa zao la minazi katika Manispaa ya Lindi kunakosababishwa na ugonjwa wa unyaufu, Serikali imeanzisha mpango maalum wa kunusuru zao hilo kwa kugawa miche bure kwa wakulima.

Kupitia mpango huo, Manispaa ya Lindi imepokea miche 12,000 ya minazi ambayo itasambazwa kwa wakulima kwa lengo la kurejesha uzalishaji na kuongeza tija katika sekta hiyo muhimu ya kilimo.

Ugawaji wa miche hiyo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Manispaa ya Lindi na Kituo cha Utafiti wa Zao la Minazi Mikocheni (Naliendele), ambacho kinatoa utaalamu na usimamizi wa kitaalamu ili kuhakikisha miche inayogawiwa inakidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa.


Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mpango huo, Meya wa Manispaa ya Lindi, Abdala Mpuluji, aliwataka watendaji wa vijiji kuhakikisha miche hiyo inawafikia walengwa waliokusudiwa na haitumiki kinyume na malengo, ikiwemo kuuzwa.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Lindi, Hudhaifa Rashid, aliwahimiza wakulima waliokabidhiwa miche hiyo kuitunza na kuihudumia ipasavyo ili kupata matokeo yaliyokusudiwa, ikiwa ni pamoja na kuinua uchumi wao binafsi na wa halmashauri kwa ujumla.


Mratibu wa zao la minazi katika manispaa hiyo alisema kuwa huu ni mara ya pili kwa halmashauri kupokea miche ya minazi. Katika awamu ya kwanza, Manispaa ilipokea miche 14,000 ambayo ilisambazwa kwa wakulima katika kata 18. Mwaka huu, imepokea miche 12,000 itakayogawiwa kwa wakulima wa kata 15.

Baadhi ya wakulima waliopokea miche hiyo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapatia miche bure, wakieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji wa zao la nazi, kuboresha kipato chao na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3