SERIKALI YA LIPA DENI LA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII NCHINI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Sangu, amesema hadi sasa Serikali imefanikiwa kulipa asilimia 95 ya deni la mifuko ya hifadhi za jamii nchini ambalo lilirithiwa kabla ya mwaka 1999, hatua ambayo imesaidia kuimarisha ukwasi na ufanisi wa mifuko hiyo katika kuwahudumia wanachama.
Akizungumza jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya Mwaka 2023, Waziri Sangu ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa utaratibu wake wa kishujaa wa kulipa deni Hilo la kihistoria la shilingi trilioni 4.46 lililokuwa linaikabili mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii nchini.
Mhe. Sangu ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya maboresho ya Sekta ya Kinga ya Jamii yaliyoanza mwaka 2018 kwa lengo la kutekeleza Ibara ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoiagiza mamlaka kuweka taratibu za kusaidia wananchi wakati wa uzee, maradhi na ulemavu.
Amesisitiza kuwa kulipwa kwa madeni hayo kumeongeza kasi ya ulipaji wa mafao kwa wakati na kuleta utulivu wa kiuchumi kwa wastaafu, huku kukiakisi dhamira ya dhati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwajali wananchi wake na kulinda haki zao za msingi.

.jpeg)
