Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
SABABU ZA WANAFUNZI KUFELI MITIHANI

SABABU ZA WANAFUNZI KUFELI MITIHANI

 

Na Angelina Mbunda – MATUKIO DAIMAMEDIA (UoI)

Walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Shule ya Moria wameeleza sababu mbalimbali zinazochangia wanafunzi kufeli katika mitihani ya ndani na nje ya shule, pamoja na athari zinazotokana na matokeo hayo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanafunzi wa shule hiyo walisema kuwa zipo changamoto nyingi zinazosababisha kushuka kwa ufaulu. Mwanafunzi Ester John Malaty alisema kuwa baadhi ya wanafunzi hufeli kutokana na kutopenda shule, kutomwelewa mwalimu darasani au kutokuwa na utaratibu wa kujisomea binafsi.

“Wanafunzi wengine hawajisomei wakiwa peke yao au hushindwa kumwelewa mwalimu, hali inayochangia kufeli kwao,” alisema Ester.

Kwa upande wake, mwanafunzi Junior Erasto alibainisha kuwa kutosikiliza kwa makini maelekezo ya mwalimu na kushindwa kuelewa maswali ya mtihani ni miongoni mwa sababu zinazosababisha kufeli.

“Wapo wanafunzi ambao hawaelewi maswali yanataka nini au hawafuatilii vizuri wanapofundishwa darasani, jambo linalowafanya washindwe kufanya vizuri kwenye mitihani,” alisema Junior.

Naye mwalimu Kandida Nzalalila alisema kuwa wanafunzi wengi hushindwa kufanya vizuri kutokana na kutojisomea na kutokuwa na uelewa sahihi wa maswali ya mtihani.

“Mwanafunzi anapaswa kuelewa swali linataka nini ili aweze kujibu kwa usahihi na ufasaha. Kukosa maandalizi kunachangia matokeo mabaya,” alieleza mwalimu huyo.

Mwalimu Adam Ngollo aliongeza kuwa uvivu wa kujisomea ni tatizo kubwa linalochangia kufeli kwa wanafunzi wengi. Alisema matokeo mabaya yanaweza kuathiri hali ya kisaikolojia ya mwanafunzi.

“Baada ya kufeli, baadhi ya wanafunzi hupata msongo wa mawazo na kuanza kujiona hawana uwezo, jambo ambalo si sahihi,” alisema.

Walimu hao walisisitiza umuhimu wa kuwapa wanafunzi ushauri na msaada wa karibu pindi wanapopata matokeo yasiyoridhisha. Walisema ni vyema walimu na wazazi kuzungumza na wanafunzi kwa upole na kuwahamasisha ili warejee katika hali yao ya kawaida na kuendelea kujitahidi, kwani kufeli si ishara ya kutokuwa na uwezo bali ni changamoto inayoweza kurekebishwa.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3