Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
OFISI YA KATIBU TAWALA MKOA WA IRINGA YAVUTIWA WA MAENDELEO YA MIKOPO ASILIMIA 10 MANISPAA YA IRINGA

OFISI YA KATIBU TAWALA MKOA WA IRINGA YAVUTIWA WA MAENDELEO YA MIKOPO ASILIMIA 10 MANISPAA YA IRINGA

 

Na Matukio Daima Media, Iringa

Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Iringa kupitia Kitengo cha Maendeleo ya Jamii imeanza rasmi zoezi la ufuatiliaji na ukaguzi wa vikundi vilivyonufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi na kuimarisha uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.


Ziara hiyo imefanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na kuongozwa na Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi, Hellena Ntahena, akifuatana na Afisa Maendeleo ya Jamii Fatuma Mohamed pamoja na Afisa Ustawi wa Jamii Ashery Mndalila.

Lengo la ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa mikopo hiyo, kufuatilia marejesho yake, pamoja na kujionea namna vikundi vinavyotumia fedha hizo katika kuendesha shughuli za maendeleo. 

Uongozi huo umefanya mazungumzo na wanufaika, kukagua miradi mbalimbali na kupokea taarifa za utekelezaji kutoka kwa maafisa husika.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Ntahena amesema Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa imejipanga kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwamba zinawanufaisha walengwa kwa kuwainua kiuchumi.



 Ameeleza kuwa mikopo ya asilimia 10 imeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambao wamekuwa wakipewa kipaumbele katika mpango huo wa kitaifa.

“Hakika tumeshuhudia mafanikio makubwa. Marejesho yanaendelea vizuri na vikundi vingi vinafanya shughuli za uzalishaji kwa ufanisi. Hii ni ishara kuwa fedha hizi zinatumika kama ilivyokusudiwa,” amesema Ntahena.

Aidha, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutenga na kutoa mikopo hiyo kwa makundi maalum, akisisitiza kuwa mpango huo unasaidia kupunguza utegemezi na kuongeza kipato kwa wananchi wa kipato cha chini. 


Amesema dhamira ya Serikali ni kuona wananchi wanajikwamua kiuchumi kupitia mikopo yenye masharti nafuu na inayolenga kukuza shughuli za uzalishaji na biashara ndogondogo.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Iringa na Mratibu wa Mikopo ya Asilimia 10, Sunday Mtamakaya, amesema tangu kufunguliwa kwa dirisha la utoaji mikopo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.7.


Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo, wanawake wamepokea shilingi milioni 889.6, vijana milioni 721.3 na watu wenye ulemavu milioni 93.3. 

Kwa mujibu wa Mtamakaya, jumla ya vikundi 154 vimenufaika, ambapo vikundi 84 ni vya wanawake, 51 vya vijana na 18 vya watu wenye ulemavu.


Ameongeza kuwa jumla ya wanufaika binafsi ni 822, wakiwemo wanawake 632 na wanaume 190. Takwimu hizo zinaonesha namna mpango huo ulivyochangia kwa kiasi kikubwa kuwainua wanawake kiuchumi, sambamba na kutoa fursa kwa vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.


Baadhi ya wanufaika walioshiriki katika kikao cha tathmini wameeleza kuridhishwa kwao na namna mikopo hiyo ilivyowasaidia kupanua biashara zao, kuongeza mtaji na kuboresha maisha ya familia zao.

 Wamesema kupitia mikopo hiyo wameweza kuanzisha na kuendeleza miradi ya ufugaji, kilimo cha mbogamboga, biashara ndogondogo pamoja na usindikaji wa bidhaa mbalimbali.


Wanufaika hao wameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa mikopo hiyo na kuahidi kuendelea kurejesha kwa wakati ili kutoa nafasi kwa vikundi vingine kunufaika.

 Wameeleza kuwa ufuatiliaji unaofanywa na Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa unasaidia kuongeza uwajibikaji na nidhamu ya matumizi ya fedha hizo.



AGIZA WINE KIWANGO YA NANASI, ALOVERA NA TANGAWIZI TOKA IRINGA PIGA SIMU 0713650634 AU 0655679553

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3