NYANYA NI NYANYASE WAFANYABIASHARA IRINGA WALIA
Na Catherin Kilwale (UoI), Matukio Daima Media
Wafanyabiashara wa nyanya katika Soko la Kitanzini, mkoani Iringa, wamelalamikia changamoto ya mvua za mara kwa mara zinazoendelea kunyesha, wakisema hali hiyo imesababisha ucheleweshaji wa bidhaa kufikishwa sokoni na hivyo kuwaletea hasara.
Wakizungumza na Matukio Daima Media, baadhi ya wafanyabiashara hao walisema miundombinu mibovu ya barabara kutoka maeneo ya uzalishaji hadi sokoni imekuwa kikwazo kikubwa, hasa katika msimu huu wa mvua.
Mfanyabiashara Zaharra Mlula alisema usafirishaji wa nyanya kutoka kwa wakulima umekuwa wa shida kutokana na mvua hizo, jambo linalosababisha bidhaa kufika sokoni zikiwa zimechelewa au kuharibika.
“Changamoto kubwa msimu huu wa mvua ni usafirishaji. Zao la nyanya halihitaji mvua nyingi kwani huathirika haraka na kuharibika, hali inayotuletea hasara,” alisema Zaharra.
Kwa upande wake, mjasiriamali mdogo Ibrahim Mbembe alieleza kuwa msimu wa mvua huambatana na changamoto nyingi katika biashara ya nyanya, ikiwemo kuharibika kwa bidhaa kabla hata ya kuifikia soko.
“Nyanya zikizidiwa na mvua huharibika na kupoteza ubora. Wateja wanakosa imani na bidhaa, na wakati mwingine hulazimika kuziacha kabisa kwa kuwa hazifai kuuzwa,” alisema.
Huku Scholar Dalu, alisema mara nyingi bidhaa hufika sokoni zikiwa tayari zimeanza kuoza, jambo linalowalazimu kuziuza kwa bei ya chini au kuzitupa.
Alisema kuwa changamoto nyingine ni wateja kuwa wabishi wanapokutana na bei zilizopanda, wakidai kuongezewa kipimo zaidi, hali inayowaumiza zaidi wauzaji.
Hata hivyo wafanyabiashara hao wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara vijijini ili kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka kwa wakulima hadi masokoni, hatua itakayosaidia kupunguza hasara na kulinda kipato chao, hususan katika msimu wa mvua.
