MCC ASAS: TUVUNJE MAKUNDI, TUJENGE UMOJA NA MSHIKAMANO
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Salim Abri Asas, amewataka viongozi wa chama waliochaguliwa katika ngazi mbalimbali kuhakikisha wanaimarisha umoja na mshikamano kwa lengo la kukijenga na kukiimarisha CCM.
Asas amesema kuwa baada ya kukamilika kwa mchakato wa uchaguzi ndani ya chama, kilichobaki sasa ni viongozi kushirikiana kwa karibu, kufanya kazi kwa bidii na kuonesha ushirikiano utakaosaidia kutekeleza majukumu ya chama kwa ufanisi.
Ametoa kauli hiyo Februari 8, 2026, wakati wa kikao maalumu na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Mufindi.
Kikao hicho kilihusisha pia viongozi wakuu wa CCM Mkoa wa Iringa, wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo, Daud Yassin.
Katika kikao hicho, Asas alisisitiza kuwa mshikamano wa viongozi ni msingi muhimu wa kuimarisha chama kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa.
Alionya migawanyiko na makundi ndani ya chama, akieleza kuwa hali hiyo inaweza kudhoofisha utekelezaji wa malengo na dira ya CCM.
Alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila kiongozi kuhakikisha anachangia kudumisha umoja, mshikamano na maadili ya chama kwa maslahi mapana ya CCM na taifa kwa ujumla.




