MBUNGE WA JIMBO LA BUKOBA MJINI APONGEZA MABORESHO YA HUDUMA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA
Na Matukio Daima Media, Kagera
Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Mhandisi Johnstone Mutasingwa amepongeza kwa dhati huduma bora naza kibingwa zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba huku akisisitiza kuwa maboresho yanayoendelea hospitalini hapo yameongeza imani ya wananchi na ubora wa huduma za afya kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera na mikoa jirani.
Pongezi hizo zimetolewa leo Februari 27, 2026 wakati Mbunge huyo alipotembelea hospitali hiyo na kuzungumza na watumishi wakiwemo madaktari, wauguzi na wataalamu wa kada mbalimbali.
Akiwahutubia, Mhandisi Mutasingwa alisema kuwa amekuwa akipokea mrejesho mzuri kutoka kwa wananchi wanaopata matibabu hospitalini hapo, wengi wakieleza kuridhishwa na huduma, weledi wa watumishi na upatikanaji wa huduma za kibingwa.
Aidha, amewahimiza watumishi wa hospitali kuendelea kushirikiana kwa karibu na uongozi wa hospitali pamoja na ofisi yake ya ubunge, ili changamoto mbalimbali za watumishi kwa ujumla (ikiwemo ajira za mkataba wa mkataba wanaootoa huduma hapo) ziweze kufikishwa sehemu husika kwa utatuzi wa haraka.
Katika hatua nyingine, Mbunge Mutasingwa ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha sekta ya afya hasa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba kupitia ajira za watumishi wapya, ujenzi wa miundombinu ya kisasa ikiwemo majengo ya Huduma za Dharura (EMD) na Wagonjwa Mahututi (ICU), pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa ikiwemo mashine ya CT-Scan.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba, George Buberwa, amemshukuru Mbunge kwa kutenga muda wa kutembelea hospitali na kuzungumza na watumishi huku akidokeza kuwa, bodi kwa kushirikiana na uongozi wa hospitali na wanaompango wa kushirikiana na wadau wa maendeleo kupanga na kutekeleza miradi ya kimaendeleo kwa lengo la kuboresha zaidi huduma za afya zaidi hospitalini hapo.
Dkt. Buberwa alitaja miongoni mwa mipango hiyo kuwa ni ujenzi wa “Private Ward” kupitia eneo la hospitali, mradi unaotarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano wa wadau wa Maendeleo wa Mkoa wa Kagera kupitia harambee.
Aliongeza kuwa Mbunge wa Bukoba Mjini ni mdau mkubwa wa maendeleo katika mkoa na akaomba kuwa wanaomba ushirikiano wakutosha wakibisha hodi ofisini kwake kwa ajili ya utekelezaji wa jambo hilo.
Naye Katibu wa Afya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba Faustine Pamba akiwasilisha taarifa ya hospitali kwa Mbunge, amesema kuwa hospitali hiyo kwa sasa inahudumia wastani wa wagonjwa wa nje 250 kwa siku, huku wagonjwa 28 wakilazwa kwa siku.













