Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MBUNGE IRINGA MJINI FADHIL NGAJILO  ATEKELEZA AHADI YA MAFUNZO KWA WAJASIRIAMALI 300

MBUNGE IRINGA MJINI FADHIL NGAJILO ATEKELEZA AHADI YA MAFUNZO KWA WAJASIRIAMALI 300

 


NA MATUKIO DAIMA MEDIA 

Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhil Ngajilo, ameanza kutekeleza ahadi yake ya kuwapatia mafunzo wajasiriamali kama alivyoahidi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa kutoa mafunzo maalum kwa wajasiriamali wapatao 300 wa jimbo hilo.


Wajasiriamali hao kutoka Manispaa ya Iringa wamenufaika na mafunzo ya siku sita yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kuendesha na kukuza biashara zao kwa tija zaidi. 

Mafunzo hayo yamewezeshwa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa lengo la kuinua uchumi wa wajasiriamali wadogo na wa kati kupitia maarifa ya vitendo na mbinu za kisasa za biashara.


Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mbunge, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Tumaini Msowoya, aliwahimiza washiriki kuyatumia ipasavyo mafunzo waliyopata, hasa katika matumizi ya teknolojia.

Alisema katika dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa wa kibiashara, teknolojia ni nyenzo muhimu ya mafanikio kwa wajasiriamali. 

Aliwataka kutumia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali kutafuta masoko mapya, kuongeza mauzo na kuwafikia wateja wengi zaidi ndani na nje ya Mkoa wa Iringa.

Kwa upande wake, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Yahaya Mpelembwa, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwainua wajasiriamali kwa kuwapatia maarifa yatakayowawezesha kusimamia biashara zao kwa ufanisi na kuongeza faida.

Alitaja maeneo yaliyofundishwa kuwa ni pamoja na masoko, usimamizi wa fedha, huduma kwa wateja na mbinu za kukuza mitaji, akieleza kuwa uelewa wa maeneo hayo ni msingi wa mafanikio ya biashara yoyote.

Naye Meneja wa Taasisi ya Star Entrepreneur General ya mkoani Morogoro, Issa Bashir, alimshukuru Mbunge huyo kwa kutoa fursa hiyo kwa wajasiriamali wa Iringa. 

Alisema washiriki walipatiwa mafunzo ya vitendo katika nyanja mbalimbali zikiwemo ufugaji wa kuku, utengenezaji wa keki, usimamizi wa biashara, kilimo cha kibiashara, utafutaji wa masoko na utengenezaji wa bidhaa ndogondogo za viwandani kama sabuni.

Imeelezwa kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Mbunge Ngajilo aliyotoa wakati wa kampeni za mwaka 2025 ya kuwajengea uwezo wajasiriamali ili kuboresha biashara zao na kuongeza kipato.


Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko kwa washiriki kwa kuwawezesha kuongeza thamani ya bidhaa zao, kupanua biashara na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Manispaa ya Iringa na Mkoa wa Iringa kwa ujumla.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3