MAJI CF NATURAL YAZINDULIWA KWA MAOMBI KANISANI
Mchungaji kiongozi wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) jimbo la Mafinga,Dayosisi ya Mufindi , Anuwai Mwinuka akiweka baraka maji CF wakati wa ibada ya shukrani ya kuagwa kwa Glory Chesco Ng'umbi binti wa mkurugenzi wa kampuni za CF Plaza Mafinga picha na Matukio Daima Media
Na Matukio Daima Media Mufindi
Uzinduzi wa kiwanda cha maji ya CF Natural umefanyika kwa namna ya kipekee baada ya kuambatanishwa na ibada maalum ya kumuaga binti wa mfanyabiashara na Mkurugenzi wa Kampuni za CF Plaza, hafla iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mafinga.
Ibada hiyo ya send-off ilifanyika jana na kuhudhuriwa na viongozi wa kanisa, waumini pamoja na wageni mbalimbali, ambapo familia ya bibi harusi mtarajiwa ilitumia nafasi hiyo kutoa shukrani ya kipekee kwa Mungu kupitia sadaka ya katoni za maji ya CF Natural.
Maji hayo yaliwekwa rasmi madhabahuni na kufanyiwa maombi maalum kama ishara ya kumrudishia Mungu utukufu na shukrani kwa baraka alizozitoa kwa familia hiyo.
Uongozi wa kanisa hilo pamoja na waumini walipongeza hatua hiyo wakisema ni mfano wa kuigwa kwa waumini wengine, kwani imeonesha namna imani inaweza kuambatana na maendeleo ya kiuchumi. Aidha walieleza kuwa uzinduzi wa kiwanda cha maji CF Natural ni hatua muhimu katika kukuza uchumi wa mji wa Mafinga na Mkoa wa Iringa kwa ujumla kupitia sekta ya viwanda.
Wakizungumza katika ibada hiyo, mchungaji Kiongozi wa usharika wa Mafinga na mkuu wa jimbo la Mafinga la Kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mufindi ,Anuwai Mwinuka na waumini wa kanisa hilo Aman Kalinga na Neema Sanga walisema licha ya tukio hilo kuwa ni sherehe ya kumuaga bibi harusi mtarajiwa, limekuwa pia baraka kubwa kwa vijana wa Mafinga na maeneo ya jirani kushuhudia fursa za ajira zitakazotokana na kuanzishwa kwa kiwanda hicho.
Walisema kiwanda hicho kinatoa matumaini mapya kwa vijana wengi waliokuwa hawana ajira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Maji CF Natural na CF Plaza, Chesco Ng’umbi, alisema pamoja na furaha ya binti yake kuolewa, ameona ni vema kumrudishia Mungu utukufu kwa kutoa sadaka ya pekee ya maji ya CF Natural yanayozalishwa mjini Mafinga.
Alisema kuwa mafanikio yote aliyoyapata ni kwa neema ya Mungu, hivyo ni wajibu wake kushukuru na kushirikisha jamii baraka hizo.
Ng’umbi aliongeza kuwa kiwanda cha maji CF Natural kimeanzishwa kwa lengo la kuchangia maendeleo ya kiuchumi, kutoa ajira kwa vijana na kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Aliahidi kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na serikali na jamii kwa ujumla katika kuhakikisha maendeleo endelevu yanapatikana.
Mbunge wa Viti Maalum Vijana Taifa, Jasmin Ng’umbi, ambaye alishiriki tukio hilo, alishukuru kwa kuanzishwa kwa kiwanda hicho na kueleza kuwa ni fursa kubwa kwa vijana.
Alisema kiwanda cha maji CF Natural ni mfano wa uwekezaji unaogusa moja kwa moja changamoto ya ajira kwa vijana, na akaipongeza familia ya Ng’umbi kwa kuwekeza nyumbani.
Hafla hiyo ya siku mbili ilionesha mchanganyiko wa imani, shukrani na maendeleo, huku ikiunga mkono juhudi za serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhamasisha na kuweka mazingira rafiki kwa uanzishwaji wa viwanda zaidi nchini ili kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi.
>





















































































