FAIDA ZA VIJANA KUJIAJIRI WENYEWE
Na Catherin Kilwale (UoI), Matukio Daima Media
Vijana wa Mtaa wa Semtema, Kata ya Kihesa mkoani Iringa, wameeleza faida za kujiajiri wenyewe kufuatia changamoto ya ajira inayowakabili wahitimu wa vyuo vikuu, huku wakitoa wito kwa vijana walioko mtaani bila shughuli rasmi kujituma na kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza na Matukio Daima, Stephano Honga, mkazi wa mtaa huo anayejishughulisha na ufundi seremala, alisema ujasiriamali umemsaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha yake na ya familia yake.
“Naweza kukidhi mahitaji yangu ya kila siku na kuhudumia familia yangu. Faida kubwa ni kwamba nasomesha watoto wangu kupitia kazi hii. Pia, hakuna anayenisimamia kwa sababu najiongoza mwenyewe katika kila hatua ya kazi yangu,” alisema Honga.
Naye Grace Bayo, mjasiriamali wa mtaa huo, aliwashauri vijana waliomaliza vyuo na wale waliopo mtaani bila ajira wasikate tamaa, bali wajitahidi kupambana kwa kutumia fursa zilizopo ili waweze kujitegemea na kuepuka utegemezi kwa wazazi au walezi.
“Sio lazima uanze na mtaji mkubwa. Ukiwa na nia na jitihada, unaweza kufanikiwa. Bila kuwa na dhamira ya dhati katika ujasiriamali, mafanikio hayawezi kupatikana licha ya changamoto zilizopo, kikubwa ni kuwa na matumaini na bidii,” alisema Grace.
Kwa upande wake, Majaliwa Mashaka, mjasiriamali anayejishughulisha na uchomeleaji vyuma, alisema ukosefu wa ajira unapaswa kuwa chachu kwa vijana kujiajiri badala ya kukaa bila kufanya chochote.
“Kujiajiri kunatupa mwamko wa kutotegemea wengine na kutokuwa mzigo kwa familia ukiwa mjasiriamali unaweza pia kusaidia wenye uhitaji na kuwashauri vijana wengine waliohitimu vyuo au walioko mtaani bila shughuli rasmi waanze kujishughulisha. Mafanikio hayaji kwa kukaa nyumbani, lazima upambane ili kufikia malengo yako,” alisema Mashaka.
Vijana hao wamehimiza taasisi na wadau mbalimbali kuendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na mitaji midogo ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kujiajiri na kuchangia maendeleo ya jamii.

