DC MBOZI AONYA WANAOKIMBIA MAREJESHO YA MIKOPO.
Na Josea Sinkala, Mbozi Songwe.
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe Mhe. Hamad Mbega, amewataka wanaufaika wa mikopo ya asilimia 10 inazotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kuzitumia kwa usahihi huku akiwaonya wanaochelewesha marejesho.
Amesema mikopo inayotolewa ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwainua wananchi kiuchumi.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo hiyo Februari 13, 2026 wilayani Mbozi, DC Mbega amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wananchi kujikwamua kupitia mitaji inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.
Katika hafla hiyo, jumla ya shilingi milioni 689 zilitolewa kwa vikundi 55 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ikiwa ni mkopo wa awamu ya pili.
DC Mbega amewapongeza wanufaika kwa kufikia hatua hiyo na kuwataka kuitumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili iweze kuleta tija katika miradi yao na kuboresha maisha ya familia zao.
“Fedha hizi ni fursa adhimu. Zikitumika kwa nidhamu na uwajibikaji, zitaleta matokeo makubwa si tu kwa vikundi vyenu bali kwa uchumi wa Wilaya yetu kwa ujumla,” alisisitiza Mbega.
Ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuwawezesha wananchi kujitegemea na kuongeza kipato kupitia shughuli halali za kiuchumi na kuwahimiza wanufaika kuendeleza utamaduni wa kurejesha mikopo kwa wakati bila kusubiri kufuatiliwa na halmashauri. Alisema lengo la Serikali si kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wakopaji, bali kuhakikisha fedha hizo zinazunguka na kuwafikia wananchi wengi zaidi wenye uhitaji.
“Kama kiongozi wa Serikali, sitarajii kuona mwananchi akichukuliwa hatua kwa kushindwa kurejesha mkopo. Ni vyema kila kikundi kikazingatia masharti ya marejesho ili kulinda heshima na uaminifu wao,” alieleza DC Mbega.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imeendelea kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa makundi maalum, hatua inayolenga kuchochea maendeleo jumuishi na kuinua ustawi wa wananchi katika wilaya hiyo.





