BEI YA MCHELE YAPANDA IRINGA.
NA EASTER KAMETA (UoI) ,MATUKIO DAIMA MEDIA
Wafanyabiashara wa mchele mkoani Iringa wamelalamikia kupanda kwa bei ya mchele, hali inayodaiwa kusababisha wao kukosa wateja na hata bidhaa kuharibika kutokana na kukaa muda mrefu bila kuuzwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, mfanyabiashara wa mchele, Joseph Shop, amesema kuwa gharama kubwa za usafirishaji wakati wa msimu wa mvua ndiyo chanzo kikuu cha kupanda kwa bei ya mchele.
Alisema kuwa mvua zinazoendelea kunyesha mara kwa mara zimesababisha miundombinu ya barabara kuwa mibovu, hali inayoongeza gharama za usafirishaji wa mchele kutoka maeneo ya uzalishaji hadi sokoni.
“Usafirishaji wa mchele msimu huu wa mvua umekuwa ghali sana, hivyo tunalazimika kuongeza bei ili angalau tupate faida kidogo,” amesema Joseph.
Kwa upande wake, mfanyabiashara mwingine, Faraja Mboma, amesema changamoto hiyo imeathiri kwa kiasi kikubwa biashara yao, huku akieleza kuwa bei ya ununuzi wa mchele imeongezeka maradufu.
“Hapo awali tulikuwa tunanunua kilo 100 za mchele kwa shilingi laki moja na elfu thelathini, lakini kwa sasa tunanunua kwa shilingi laki mbili hali hii inatufanya tushindwe kupata faida,” amesema Faraja.
Nao wateja hawajasalia nyuma katika kuzungumzia hali hiyo.
Dorin Lusinde, mkazi wa Iringa, amesema kuwa kwa sasa mchele umekuwa kama dhahabu kutokana na bei yake kupanda sana.
“Mchele kwa sasa umekuwa kama dhahabu hapa Iringa, Wananchi wa kipato cha chini tunapata ugumu mkubwa kuununua Zamani kilo moja ilikuwa shilingi 2,000, lakini sasa ni kati ya shilingi 3,000 hadi 3,500,” amesema Dorin.
Royd Sanga alisema kuwa awali bei ya mchele ilikuwa rafiki kwa wananchi wengi, lakini kwa sasa hali imekuwa tofauti.
“Zamani ilikuwa rahisi mtu kununua hata kilo 30 za mchele, lakini kwa bei za sasa huwezi kumudu, tunalazimika kununua kilo chache tu,” amesema Royd.
Kupanda kwa bei ya mchele mkoani Iringa kumeendelea kuwa changamoto kwa wafanyabiashara na wananchi, huku wengi wakiiomba serikali kuchukua hatua za kudhibiti gharama za usafirishaji na kuweka bei elekezi ili kulinda maslahi ya walaji.

