BALOZI SIRRO AONYA WAZAZI WASIOSIMAMIA ELIMU YA WATOTO WAO
Feb 9, 2026
MKUU wa mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro amewatupia lawama wazazi kuwa ni changamoto kubwa kwa kuendelea kwa utoro sugu kwa wanafunzi kwa kushindwa kutimiza wajibu wao katika kusimamia elimu ya watoto wao.
Balozi Sirro alisema hayo katika mkutano na waandishi wa habari na viongozi waandamizi wa mamlaka za serikali za mitaa kuhusu kampeni ya umasishaji wa uandikishaji wa watoto walio nje ya mfumo rasmi na kuwarudisha shuleni walioacha shule inayoendeshwa na serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF).
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa pamoja na mipango mingine inayofanywa na serikali na wadau bado haitoshi kama wazazi hawatakuwa tayari kuwasimamia watoto wao kwenda shule na kuacha shughuli nyingine ambazo watoto hao wanazifanya na kuacha masomo na kwamba pamoja na umasishaji na jitihada nyingine pia sheria ya elimu itatumika kuwasimamia wazazi kutekeleza wajibu wao.
Akizungumza katika mkutano huo Katibu Tawala wa mkoa Kigoma,Hassan Rugwa alisema kuwa pamoja na changamoto ya mdondoko mkubwa kwa wanafunzi wa shule za msingi lakini mkoa huo umefanya vizuri kitaaluma katika matokeo ya shule za msingi na sekondari na mkoa huo kushika nafasi za juu kwenye mambo mbalimbali ya kitaaluma.



