Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 WIZARA YA MADINI YAJENGA MAABARA KUBWA YA KISASA DODOMA

WIZARA YA MADINI YAJENGA MAABARA KUBWA YA KISASA DODOMA


Na Hamida Ramadhan Matukio Daima Media Dodoma

WIZARA  ya Madini imetangaza ujenzi wa Maabara kubwa ya kisasa katika eneo la Nala, mkoani Dodoma, kwa lengo la kusaidia upimaji na utoaji wa taarifa sahihi za sampuli za madini.

Maabara hiyo inatarajiwa kuwa kitovu cha utoaji wa huduma za madini kusini mwa Jangwa la Sahara.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema hayo leo Januari 26,2026 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha pili cha Awamu ya Sita ya Serikali.


Amesema kuwa ujenzi wa maabara hiyo utaleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa Tanzania na nchi jirani, sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani. 

Aidha, Wizara imeingia makubaliano na GST ili taasisi hiyo iwe kitovu cha utoaji huduma za maabara kusini mwa Jangwa la Sahara.


Katika kuongeza thamani ya madini, Waziri Mavunde amebainisha kuwa Wizara inaendelea kwa kasi na ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani, ambapo hadi sasa vipo viwanda sita (6) vya kusafisha dhahabu pamoja na viwanda vingine vya madini mbalimbali.

Kwa upande wa utoaji wa leseni, Wizara ya Madini inaelekea kutumia mfumo wa E-Licensing, ambao hautahitaji waombaji kufika wizarani. Kupitia mfumo huo, mwombaji atapatiwa leseni na ndani ya kipindi cha miezi mitatu atatakiwa kuwasilisha taarifa ya utafiti wake.

"Wizara imefanikiwa kuratibu utoaji wa leseni 12,130, sawa na asilimia 117.8 ya lengo la mwaka wa fedha 2024/2025. Aidha, katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, jumla ya leseni 8,418 zilitolewa sawa na asilimia 147 ya lengo la kipindi husika,"  Amesema Waziri Mavunde 



Na kuongeza " Kuanzia Novemba 2025 hadi Januari 2026, leseni 2,376 zilitolewa ambapo katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, Wizara ilifuta leseni 73 za utafutaji na uchimbaji madini kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo kutokuendelezwa kwa maeneo husika, " Amesema


Aidha ameeleza kuwa Baadhi ya maeneo yaliyokuwa na leseni hizo yatatengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo, pamoja na Vijana na Wanawake wanaoshiriki katika programu ya Mining for Brighter Tomorrow (MBT).



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3