Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WANANCHI WAMETAKIWA KUJITOKEZA KUSHIRIKI UZINDUZI WA MELI YA MV NEW MWANZA.

WANANCHI WAMETAKIWA KUJITOKEZA KUSHIRIKI UZINDUZI WA MELI YA MV NEW MWANZA.

NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

Wananchi wa Mkoani Mwanza wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Lameck Mwigulu Nchemba, katika uzinduzi wa meli ya MV New Mwanza, baada ya kukamilika kwa mradi huo mkubwa wa kimkakati.


Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Omary Mtuwa, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukamilisha mradi huo ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ndani ya mkoa huo.

Mtuwa ameleza kuwa  meli hiyo ilipokelewa ikiwa imekamilika kwa asilimia 40, lakini serikali ya awamu ya sita iliikamilisha kwa asilimia 60 iliyobaki hadi kufikia hatua ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla.

“Meli ya MV New Mwanza itakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kwani itarahisisha usafiri wa majini, kukuza uchumi na kuongeza fursa za kibiashara kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza,” alisema Mtuwa.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nyamagana, Wilaya ya Nyamagana, Dkt. Frank Chacha, alisema meli hiyo iliyogharimu takribani shilingi bilioni 120 imekamilika na sasa iko tayari kuanza kutoa huduma.

Amefafanua kuwa meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 1,200, mizigo tani 400, magari madogo 20 na magari makubwa matatu, hali itakayofungua fursa mpya za kiuchumi kwa wakazi wa Nyamagana na Kanda ya Ziwa kwa ujumla.

“Kwa kuwa meli hii ipo Nyamagana, tutaona ongezeko la shughuli za kibiashara, siyo tu katika soko la Mwanza bali pia katika bandari zote itakazopita ikiwemo Bandari ya Kemondo,” alisema Dkt. Chacha.

Aliongeza kuwa ujenzi wa meli hiyo umeongeza ujuzi kwa vijana na wataalamu wa ndani, kwani asilimia 100 ya wataalamu wa Kitanzania walishiriki katika ujenzi wake, hali iliyoleta ajira za moja kwa moja na kuandaa fursa zaidi za ajira zitakapoanza shughuli za uendeshaji wa meli hiyo.


Dkt. Chacha pia aliwataka wananchi kudumisha mshikamano na uaminifu, hasa kwa wale watakaopata ajira katika meli hiyo, ili kuhakikisha maendeleo endelevu yanapatikana.

Naye Cuthbet Albert, mdau wa maendeleo, alisema ameridhishwa na juhudi za serikali kukamilisha meli ya MV New Mwanza, akieleza kuwa ni meli ya kisasa itakayoongeza thamani katika kukuza uchumi wa Mwanza na taifa kwa ujumla.




Aidha Albert akielezea kuwa meli hiyo itaongeza kipato kwa wafanyabiashara na kurahisisha usafirishaji wa mizigo kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani.


“Tunaposema Mwanza ni kitovu cha uchumi wa Kanda ya Ziwa na Afrika Mashariki, maana yake mfanyabiashara kutoka Geita anaweza kutumia meli hii kusafirisha mizigo hadi Mwanza au Kenya kwa haraka na usalama zaidi,” alisema Albert.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3