WAGONJWA 2000 KUFANYIWA UPASUAJI WA MABUSHA, MILIONI 992 KUTUMIKA.
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
SERIKALI imepanga kufanya upasuaji wa mabusha kwa wagonjwa 2,000 katika mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo hadi sasa wagonjwa 1,700 wamepangiwa kufanyiwa upasuaji kwa gharama ya shilingi Milioni 992, fedha zinazotolewa na Serikali.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa, Januari 30, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Duniani.
Waziri Mchengerwa amesema walengwa wa huduma hiyo watatoka katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro na Mbeya.
Amesema Serikali, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, itaendelea kutoa huduma kwa wananchi wanaoathirika na magonjwa hayo, ikiwemo huduma za upasuaji.
“Katika mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya wananchi 1,084 wamepatiwa huduma ya upasuaji wa mabusha nchini,” amesema Mchengerwa.
