Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
UHIFADHI WA MAZINGIRA WATAJWA KUVUTIA WAFANYABIASHARA TUNDUMA

UHIFADHI WA MAZINGIRA WATAJWA KUVUTIA WAFANYABIASHARA TUNDUMA

 


Na Moses Ng’wat, Tunduma

Uhifadhi na uboreshaji wa mazingira umetajwa kuwa nguzo muhimu katika kuvutia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi katika mji wa mpakani wa Tunduma, wilayani Momba, mkoani Songwe.


Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Mwandobo, Januari 27, 2026, wakati akiongoza zoezi la upandaji wa miti zaidi ya 200 katika eneo la Shule ya Sekondari Danida, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.



Mwandobo amesema mji wa Tunduma ni lango muhimu la kibiashara za kimataifa na unapokea wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo ni wajibu wa wananchi na viongozi kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa kupanda miti mingi hali itakayosaudia kwa kiwango fulani kuvutia wafanyabiasha.


“Upandaji na utunzaji wa miti siyo tu suala la mazingira, bali ni uwekezaji wa muda mrefu kwa uchumi wa mji wetu kwani miti husaidia kuzalisha hewa safi, kutoa kivuli, kupunguza vumbi na kuboresha hali ya hewa kwa ujumla,” amesema Mwandobo.


Ameongeza kuwa mazingira safi na salama huongeza mvuto wa uwekezaji na wafanyabiashara, huku akiwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa miti iliyopandwa ili iwe na manufaa ya kudumu.


Zoezi hilo limewakutanisha makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo madereva wa bodaboda, madiwani, wafanyabiashara, wanafunzi pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mariam  Chaurembo.

Washiriki wa zoezi hilo wameeleza kuwa upandaji miti ni hatua muhimu katika kulinda mazingira ya mji wa Tunduma unaokua kwa kasi, huku wakiahidi kuendeleza utamaduni wa kupanda na kutunza miti katika maeneo yao ya kazi na makazi.


Naye, Afisa mazingira wa Halmashauri ya mji, Azizi Mayota, akitoa taarifa ya uhifadhi mazingira amesema kwa mwaka wa fedha wa 2025/26 Halmashauri ilizalisha miche 635,000 ya miti mbalimbali ikiwemo ya matunda ikiwa ni utekeleza maagizo ya serikali ya kuhakikisha kila Halmashauri inapanda miti 1,500,000 kwa mwaka.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3