PHOCAS AONGOZA KAMATI YA FEDHA MISSENYI KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO, ASISITIZA KUBANA MATUMIZI
Kamati ya fedha Utawala na Mipango (FUM) Halmashauri ya Wilaya Missenyi imekagua miradi 6 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 574.9
Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Missenyi Diwani wa Kata Bwanjai Phocus Rwegasira imekagua miradi hiyo Januari 26, 2026 ili kujiridhisha na thamani ya fedha zilizotolewa na serikali kwa kuangalia viwango na ubora wa miradi husika
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo Phocus Rwegasira amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wake baraza la Madiwani litahakikisha linasimamia vizuri miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za serikali ili iendane na viwango vilivyokusudiwa pia akasisitiza umuhimu wa kubana matumizi ili kubakiza chenji
Aidha amesema kuwa kamati ya FUM imeelekeza wasimamizi wa miradi iliyokaguliwa kuhakikisha wanarekebisha mapungufu yaliyobainiwa na kamati sambamba nakukamilisha miradi hiyo kwa wakati
Baadhi ya miradi iliyokaguliwa ni mradi wa ujenzi wa madarasa matatu na matundu 6 ya vyoo shule ya msingi Kajunguti,ukamilishaji wa bweni katika shule ya sekondari Kikukwe Kanyigo na ukamilishaji wa zahanati ya Bukabuye
Miradi mingine iliyokaguliwa ni ukamilishaji wa bwalo katika shule ya sekondari BWABUKI,ujenzi wa madarasa shule ya msingi Novath Rutageruka na ujenzi wa madarasa 3 shule ya msingi Kayanga iliyoko Kata Kitobo.
