Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
RDO, MBUNGE MUFINDI KASKAZINI WATOA MSAADA KWA WAATHIRIKA WA KIMBUNGA MDABULO

RDO, MBUNGE MUFINDI KASKAZINI WATOA MSAADA KWA WAATHIRIKA WA KIMBUNGA MDABULO


NA MATUKIO DAIMA MEDIA

Shirika la Rural Development Organization (RDO) kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, Exaud Kigahe, pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo, limetoa msaada wa haraka kwa wananchi wa Kata ya Mdabulo, Wilaya ya Mufindi, waliokumbwa na athari za mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali, hali iliyosababisha nyumba kuezuliwa mapaa na nyingine kuharibiwa kabisa.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Mkurugenzi wa RDO Fidelise Filipatali alisema janga hilo lililoanza Jumapili lilisababisha uharibifu wa nyumba takribani 17 katika vitongoji mbalimbali vya kata hiyo, na kuwaacha baadhi ya wakazi bila makazi salama.

“Mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali zilisababisha nyumba kadhaa kuezuliwa mapaa na kuharibu sehemu za kulala pamoja na vyakula hivyo, RDO kwa kushirikiana na wadau wengine tumeanza mara moja shughuli za ujenzi na ukarabati ili kurejesha matumaini kwa wananchi,” alisema Filipatali.


Alieleza kuwa lengo kuu la RDO ni kuhimiza miradi ya kujiletea maendeleo vijijini, ikiwemo kuwajengea uwezo vijana wa maeneo husika kupitia vyuo vya ufundi, ambao kwa sasa wamekuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zinazojitokeza katika jamii zao.


“Vijana wetu tayari wapo kazini hii inaonesha dhahiri kuwa mafunzo tunayotoa yanarejesha matokeo chanya, kwani kabla hata ya kusubiri msaada wa serikali, baadhi ya nyumba zilianza kufanyiwa ukarabati siku ileile janga lilipotokea,” aliongeza.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mdabulo, Marko Shayo, alishukuru shirika la RDO kwa mchango wao wa haraka na ushirikiano mzuri waliouonesha katika kukabiliana na janga hilo.


“Tukio lilitokea Jumapili mchana kuelekea jioni mvua kubwa iliyoambatana na upepo iliezua mapaa ya nyumba na nyingine kubomoka kabisa bahati nzuri hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa tunawashukuru sana RDO kwa kuja mapema na kuleta timu ya wanafunzi kusaidia kurejesha miundombinu,” alisema Shayo.

Diwani Shayo pia alieleza mchango mkubwa wa Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Exaud Kigahe, ambaye ametoa zaidi ya bati 100 kwa ajili ya kusaidia ujenzi na ukarabati wa nyumba zilizoharibiwa.

Naye Afisa Tarafa wa Ifwagi, Faraja Ndapo, alisema tathmini ya kina imefanywa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na kubainisha kuwa Kata ya Mdabulo ndiyo iliyoathirika zaidi.


“Tumekaa na kuweka mikakati ya kuhakikisha waathirika wanarejea katika makazi yao tayari tumewasiliana na wadau na Halmashauri imeahidi kutoa msaada tunashukuru RDO kwa mchango wao mkubwa, kwani hata katika Tarafa ya Ifwagi wamekuwa wakisaidia watoto yatima na makundi yenye uhitaji,” alisema Ndako.


Kwa upande wa waathirika, Hezron Myengu, mkazi wa Mdabulo, ameushukuru uongozi wa kata, wilaya na wadau kwa msaada walioutoa.
“Tulikuwa katika hali mbaya sana, kila kitu kiliharibika na tulibaki nje Lakini kwa jitihada za viongozi na wadau, baadhi ya nyumba tayari zimeanza kukarabatiwa,” amesema.


Naye Klensenzia Lumungo, muathirika mwingine, amesema tukio hilo lilitokea ghafla wakati akiwa ndani na watoto wake.


“Paa lilipeperuka na kuanguka uwanjani, maji yakaingia ndani na kila kitu kikaanza kuelea.
 Tunashukuru Mungu hakuna aliyepata madhara, na tunawashukuru wadau wote waliokuja kutusaidia,” alisema.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3