MAVUNDE ATOA VIFAA VYA MICHEZO KWA MITAA 104 MTUMBA
Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media,Dodoma
WAZIRI wa Madini na Mbunge wa Mtumba, Anthony Mavunde, ametoa vifaa vya michezo kwa mitaa 104 ya jimbo la Mtumba ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha michezo ya jamii na kuibua vipaji vya vijana, sambamba na maandalizi ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha kukuza na kuendeleza vipaji vya soka kupitia programu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Mavunde amesema tayari wameanza mazungumzo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili Mtumba iwe miongoni mwa maeneo yatakayofaidika na programu za FIFA zinazolenga kuendeleza soka la vijana, hatua itakayosaidia kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Amesema Serikali na Ofisi yake ya Mbunge itaendelea kuboresha na kufanya marekebisho ya viwanja vya michezo katika mitaa mbalimbali, ili kuhakikisha kila kijana mwenye kipaji anapata mazingira salama na rafiki ya kuendeleza uwezo wake, badala ya vipaji hivyo kupotea kutokana na ukosefu wa miundombinu.
Katika hatua nyingine, Mavunde amewataka wenyeviti wa mitaa kwa kushirikiana na madiwani kuhakikisha wanalinda maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya michezo, akisisitiza kuwa maeneo hayo ni urithi wa kizazi kijacho na hayapaswi kuvamiwa au kubadilishwa matumizi.




