Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
CHUO CHA NIT CHAWAFUNDA WAHITIMU WAKE

CHUO CHA NIT CHAWAFUNDA WAHITIMU WAKE

Na Matukio Daima Media

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kimesema tafiti zinazofanywa kwa wahitimu wa chuo hicho zinaonyesha kuwa wahitimu wa chuo hicho wamekuwa wakipata ajira na kujiajiri kutokana na umahiri wanaotoka nao chuoni hapo.

Hayo yalisemwa jana chuoni hapo na Mkurugenzi wa Taaluma wa chuo hicho,Eva Omari wakati wa kongamano la kuwapa ujuzi wahitimu wa chuo hicho mwaka huu, kuhusu mambo yanayohitajika kwenye jira.

Kwenye kongamano hilo wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu walitoa mada mbalimbali  za kuwapa ujuzi zaidi wahitimu hao kuhusu namna ya kujitambulisha, kujiamini na namna ya kuenenda baada ya chuo.

Eva alisema wanafunzi wanaopewa ujuzi ni wanafunzi wa mwaka wa tatu ambao wanatarajiwa kuhitimu kozi mbalimbali na kuingia kwenye soko la ajira kufanya kwa vitendo yale waliyofundishwa chuoni.

“Tuko hapa na wataalamu mbalimbali kuhakikisha wanawapa ujuzi ili wanapoingia kwenye soko la ajira hawababaiki, ingawa wamekaa chuo kwa miaka mitatu lakini kuna ujuzi ambao ni muhimu wasipoupata hata kule kwenye ajira ni changamoto,” alisema

“Tunawaandaa ili wanapokwenda kwenye soko la ajira wanakuwa wanakubalika, wanakuwa na mwenendo mzuri kiasi cha kuwafanya waajiri waone kweli wamepata watumishi, wanafundishwa pia masuala ya maadili sehemu za kazi na mambo mengine,” alisema Eva

Alisema wataalamu hao kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wamekuwa wakiwapa mafunzo wahitimu wa chuo hicho kila mwaka ili waweze kuwa wabunifu kwenye maeneo yao ya kazi wanapohitimu.

“Siku ya leo tumeitenga kuhakikisha wanaohitimu mwaka huu tunawaandaa kisaikolojia, tunajua kuwa dunia ya leo haihitaji tu taaluma uliyonayo inakwenda mbali zaidi ya hapo, sasa usipowaandaa wanakumbatana na changamoto mbalimbali kwenye ajira,” alisema

Alisema program hiyo ya kuwaandaa wahitimu hufanyika kila mwaka na kwamba huu ni mwaka wa tatu tangu waianzishe na imeonesha mafanikio makubwa sana.

“Huwa tunafanya tafiti kujua wahitimu wetu wako wapi na wanafanya nini, tumebaini kuwa wanaoajiriwa ni wengi zaidi na wanapokuwa kwenye mazoezi ya vitendo waajiri wanatupa taarifa kuwa wanafunzi wetu wanafanya vizuri huko waliko,” alisema

“Tumebaini kuwa zaidi ya asilimia 50 wahitimu wetu wanaajiriwa kwenye kampuni na taasisi mbalimbali na wengine wanajiajiri wenyewe, tuna kozi nyingi kama ya ujasiriamali sasa kozi kama hii inawasaidia sana kujiajiri wengine wakiwa hapahapa chuoni wanaanza kufanya biashara wakimaliza wanakuwa na ujasiri wa kuanzisha biashara,” alisema

Naye Suzan Patrick ambaye ni Ofisa Kazi Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema majukumu yao ni kuwapa ujuzi wahitimu watarajiwa ili wasikumbane na changamoto kwenye maeneo ya ajira.

“Tunafahamu vyuoni wanafundishwa taaluma zao lakini tuna ujuzi wa kawaida ambao haufundishi darasani sasa sisi kupitia kitengo chetu cha huduma za ajira ni jukumu letu kuwapatia vijana ujuzi huo ili uwasaidie wanapoenda kutafuta kazi,” alisema


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3