BUNGE BONANZA: WASHIRIKI WATAJITOELEA KUCHANGIA DAMU SALAMA
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
MWENYEKITI wa Bunge Bonanza, Festo Sanga, amesema washiriki wa Bunge Bonanza wanatarajiwa kujitolea kuchangia damu salama kwa hiari katika tukio litakalofanyika Jumamosi, Januari 31, 2026, kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari John Merlin Miyuji jijini Dodoma.
Akiongea na waandishi wa habari leo Januari 29 ,2026 Bungeni jijini Dodoma Sanga amesema zoezi hilo lina lengo la kuokoa maisha ya wagonjwa, kupunguza dharura za kiafya na kuimarisha mshikamano wa kijamii kati ya washiriki na jamii kwa ujumla.
Ameeleza kuwa kuchangia damu ni kitendo cha huruma kinachoongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa afya na mshikamano wa kitaifa.
Amesema Bunge Bonanza linahusisha mashindano ya michezo ya burudani ikiwemo mpira wa miguu, kuruka kamba, pete, mashindano ya kula, kufukuza kuku pamoja na michezo mingine yenye lengo la burudani na mshikamano.
Ameongeza kuwa tukio hilo litawakutanisha mashabiki wa timu za soka za Simba na Yanga, washiriki kutoka vyuo mbalimbali pamoja na Wizara za Kilimo, Ulinzi na Vijana.
Amefafanua kuwa washiriki wote, wakiwemo wabunge na watumishi wa Bunge, wataanza matembezi ya pamoja kuanzia saa 12:00 asubuhi jirani na Chuo cha Mipango Dodoma kabla ya kuanza kwa michezo rasmi.
Amesema shughuli za michezo na burudani zitaambatana na utoaji wa zawadi maalum kwa washiriki watakaoshinda, jambo linalosaidia kuongeza hamasa na mshikamano.
Kwa upande wake, Meneja Mahusiano wa Azania Benki, Elizabeth Nyayega, amesema benki hiyo imeendelea kudhamini bonanza hilo kwa kutoa vifaa vya michezo na huduma nyingine za kimfumo pamoja na huduma za kibenki kwa washiriki na jamii.
Amesema ushiriki wa Azania Benki kama mdhamini mkuu wa bonanza hilo unalenga kuhimiza faida za michezo ikiwemo kuboresha afya, mshikamano wa kijamii, malezi kwa vijana na maendeleo endelevu ya jamii.
Naye shabiki wa Simba, Julian Hamoga, ameshauri utoaji wa nishani ufanyike kwa utaratibu mzuri zaidi ili kuhakikisha burudani inaendelea kwa mpangilio mzuri.
Bunge Bonanza linaendelea kuwa jukwaa la mshikamano wa kijamii, burudani na malezi, likiimarisha mshikamano wa kitaifa kati ya mashabiki, wabunge, watumishi wa Bunge na wadau wa jamii, huku likichangia maendeleo endelevu ya michezo na ustawi wa kijamii jijini Dodoma na Tanzania kwa ujumla.
Hata hivyo katika tukio hilo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Bunge Bonanza hilo.
Mwisho






