WAFANYABIASHARA KUUNGANISHWA NA FURSA ZA UWEKEZAJI
NA CHAUSIKU SAID MATUKIO DAIMA MWANZA
Chama cha Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT), kwa kushirikiana na Benki ya Azania, kimeandaa jukwaa litakalowaunganisha wafanyabiashara, wananchi na wadau mbalimbali na fursa za uwekezaji kupitia Mkutano Mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika jijini Mwanza.
Jukwaa hilo linatarajiwa kuwawezesha washiriki kupata maarifa mapya ya kibiashara, kubadilishana uzoefu, kujenga mitandao ya kibiashara na kutambua fursa za uwekezaji zinazoweza kusaidia kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Mwenyekiti wa ALAT Taifa, ambaye pia ni Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine kwa kushirikiana na Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa, ambaye pia ni Meya wa Jiji la Mbeya, Dormohamed Issa, wamewataka wananchi wa Mwanza na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki mkutano huo ili kutumia fursa zitakazotolewa.
Wamesema ushiriki wa wananchi na wafanyabiashara ni muhimu katika kunufaika na fursa za kiuchumi zitakazojadiliwa, pamoja na kujenga mahusiano na wadau mbalimbali yatakayoweza kufungua milango ya maendeleo ya biashara na uwekezaji.
Akizungumzia ushiriki wa Benki ya Azania katika mkutano huo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa na Biashara za Serikali wa benki hiyo, Samson Mahimbi, amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kuwawezesha wananchi na wafanyabiashara kupata maarifa mapya, kutambua fursa za biashara na kuimarisha mahusiano baina ya wadau.
Amesema kupitia jukwaa hilo, washiriki watapata nafasi ya kujifunza na kubadilishana uzoefu utakaoweza kuwasaidia kuboresha shughuli zao za biashara na kutumia fursa zilizopo katika mazingira yao.
Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano ya Biashara za Serikali wa Benki ya Azania, Grece Ngoma, amesema benki hiyo imewaalika wananchi pamoja na taasisi za serikali kushiriki mkutano huo ili kupata uelewa kuhusu huduma mbalimbali za kifedha zinazoweza kuwasaidia katika utekelezaji wa miradi yao ya maendeleo.
Amesema huduma hizo ni sehemu ya mchango wa benki hiyo katika kuwawezesha wadau mbalimbali kutumia fursa za kifedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Viongozi hao wameeleza kuwa mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa la kuimarisha ushirikiano kati ya serikali za mitaa, sekta binafsi na wananchi katika kuchochea uwekezaji na kukuza uchumi.