VIKUNDI 43 VYANUFAIKA NA MKOPO WA MILIONI 262 HALMASHAURI YA SAME.
Nov 13, 2026
SAME.
HALMASHAURI ya wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro imetoa mikopo yenye jumla ya Shilingi Milioni 262 kwa vikundi 43 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kupitia mpango wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri, kwa lengo la kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi na kukuza shughuli zao za uzalishaji.
Katika mgawanyo wa fedha hizo, vikundi 28 vya wanawake vimepatiwa Shilingi Milioni 160, vikundi 11 vya vijana vimepatiwa Shilingi Milioni 87, huku vikundi vinne vya watu wenye ulemavu vikikabidhiwa Shilingi Milioni 15.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, aliwasisitiza wanufaika kuhakikisha wanatumia fedha hizo kwa malengo yaliyowasilishwa wakati wa maombi ya mikopo na kuzirejesha kwa wakati ili kuwawezesha wananchi wengine kunufaika na fursa hiyo.
“Fedha hizi mnazopokea siyo msaada, ni mkopo na mnatakiwa kuzitumia kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi na si kwenda kuzitumia nje ya malengo mliyoyaainisha, lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanajikwamua kiuchumi pia kumbukeni kuzirejesha kwa wakati ili na wengine waweze kunufaika,” alisema Kasilda.
Aidha, aliwaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha vikundi ambavyo havikupata mikopo hiyo vinapatiwa elimu na kujengewa uwezo kuhusu namna bora ya kuandaa na kuwasilisha maombi ya mikopo, ili viweze kunufaika katika awamu zinazofuata kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Maendeleo ya jamii Halmashauri ya Wilaya ya Same, Ally Msumi alisema Halmashauri imejipanga kukabiliana na changamoto za mfumo wa maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kwa kuandaa vishikwambi 26 vitakavyotumiwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kata zote za wilaya hiyo kuwasaidia wananchi kuwasilisha maombi yao, ambapo hadi sasa vishikwambi 17 tayari vimenunuliwa.
Kwa upande wa wanufaika wa mikopo hiyo waliishukuru Serikali kwa kuwapatia fursa hiyo ya kuwawezesha kiuchumi, huku wakiahidi kutumia fedha hizo kwa shughuli walizokusudia na kuhakikisha wanazirejesha kwa wakati ili kuendeleza mpango huo na kutoa nafasi kwa vikundi vingine kunufaika.


