TARURA YATENGA SH. MILIONI 887 KWA VIKUNDI 41 SINGIDA VITAKAVYOTEKELEZA MPANGO WA CBRM
Nov 14, 2026
Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
JUMLA ya Sh milioni 887.4 zimetengwa katika Mkoa wa Singida kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli za matengenezo ya kawaida ya miundombinu ya barabara, kupitia Mpango wa Community Based Routine Maintenance (CBRM) unaotekelezwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Kupitia mpango huo, zaidi ya vikundi 41 vinanufaika kiuchumi kwa kupata fursa za ajira na kujipatia kipato kupitia kazi mbalimbali za utunzaji wa miundombinu ya barabara, ikiwamo usafi wa maeneo ya barabara na shughuli nyingine za matengenezo ya kawaida.
Mratibu wa Mpango wa CBRM Mkoa wa Singida, Mhandisi Gisela Maro, akizungumza juzi na waandishi wa habari alisema mpango huo umekuwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, kuongeza kipato na kuimarisha ushiriki wa jamii katika shughuli za maendeleo.
Alisema mbali na kuwapatia wanavikundi ajira na kipato, mpango huo pia unalenga kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika kusimamia usafi na utunzaji wa miundombinu inayowazunguka.
" Kupitia mpango huu, wananchi wanapata ajira na kipato, lakini kubwa zaidi tunawajengea vikundi uwezo wa kusimamia usafi na utunzaji wa maeneo yao wenyewe," alisema Mhandisi Maro.
Akifafanua mgawanyo wa fedha hizo, alisema Halmashauri ya Wilaya ya Iramba imetengewa Sh milioni 382.5, Mkalama Sh milioni 122.4, Singida Manispaa Sh milioni 191.25 na Halmashauri ya Wilaya ya Singida Sh milioni 191.25.
Alisema mpango huo ulianza kutekelezwa Oktoba Mosi mwaka huu na unaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa lengo la kuhakikisha vikundi vilivyolengwa vinapata fursa ya kushiriki katika shughuli hizo na kunufaika na fedha zinazotengwa na Serikali.
Mhandisi Maro alifafanua kuwa fedha hizo ni sehemu ya asilimia 30 ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuwawezesha vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli za matengenezo ya kawaida ya miundombinu ya barabara.
Alisema utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa wanavikundi, ikiwamo kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira, kuongeza kipato cha familia na kuwapa nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika shughuli za maendeleo.
Aidha, alksema ushiriki wa vikundi hivyo katika utunzaji wa barabara utasaidia kuimarisha mazingira ya miundombinu hiyo na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuitunza ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa jamii.
Kwa upande wa wanufaika, walisema mpango huo ni fursa muhimu kwao kujikwamua kiuchumi, kwani unawawezesha kupata kipato kupitia nguvu na muda wanaoutumia katika kufanya kazi za utunzaji wa barabara.
Walisema kabla ya kupata fursa hiyo, baadhi yao walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira na mitaji ya kuanzisha shughuli za kujipatia kipato, lakini kupitia ushiriki wao katika mpango huo wanapata nafasi ya kufanya kazi na kujiongezea
"Mpango huu umewapa nafasi ya kutumia vikundi vyao kama nyenzo ya maendeleo, huku ukiwajengea uzoefu wa kufanya kazi kwa ushirikiano, uwajibikaji na kusimamia shughuli zinazoweza kuwanufaisha kiuchumi,," walisema.
Aidha,wameiomba Serikali kuendelea kuutekeleza na kuupanua mpango huo ili vikundi vingi zaidi viweze kunufaika, hususan vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ambao wanahitaji fursa za ajira na uwezeshaji wa kiuchumi.
Kwa ujumla, mpango wa CBRM unaunganisha juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya barabara na uwezeshaji wananchi kiuchumi, huku ukitoa nafasi kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kuwa sehemu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.



